Longido. Waziri wa Maji wa Tanzania, Jumaa Aweso amewaambia Longido, Serikali ipo mbioni kutangaza zabuni ya kumpata mkandarasi atakayetekeleza mradi wa kupeleka maji ya uhakika eneo la Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Aweso ameeleza hayo baada ya kupigiwa simu na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla aliyempigia simu kutaka kujua mipango ya Serikali ya kutatua kero hiyo, baada ya uongozi wa chama hicho wa wilaya na Mbunge wa Longido, Dk Steven Kiruswa kutoa kilio hicho.
“Mheshimiwa Mwenezi (Makalla) pamoja mambo mazuri yanayotekelezwa na Serikali hapa tuna changamoto ya maji, hapa katika mji wa Longido na Namanga unaongoza kuwa wingi wa watu, fedha zimeshatengwa tunaomba uendelee kusukuma ili zitolewe zikatekeleze mradi.
“Mradi wa maji yanatoka Mto Simba mkoani Kilimanjaro yakifikishwa Longido yasambazwa hadi Namanga, lakini hayatoshelezi, lakini Serikali imetenga Sh14 bilioni kwa ajili ya mradi maji utakaowezesha kupatikana lita nyingi za maji kwa siku yatakayopelekwa Namanga,” amesema Dk Kiruswa ambaye ni Naibu Waziri wa Madini.
Leo Alhamisi Septemba 5, 2024, akizungumza katika cha ndani na viongozi wa CCM wilayani Longido na baadhi ya mkoa wa Arusha, Makalla alitumia nafasi hiyo kumpigia simu Aweso ili kupata majibu ya Serikali ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Namanga.
Katika majibu yake, Aweso amesema mahitaji ya maji Namanga ni lita 1.6 milioni lakini uwezo uliopo wa kuzalisha huduma hiyo ni lita 800,000, ndiyo maana Serikali ikajenga kisima eneo la Sinya kitakachozalisha maji lita 2milioni.
“Tumeshapata idhini ya kutekeleza mradi huo, niwaambie tutautekeleza sasa hivi tunaanza kuutangaza ili kumpata mkandarasi na baada ya vikao vya Bunge kuisha nitakuja Longido kuwapa taarifa kuhusu kuanza kwa mradi huu wa kupeleka maji Namanga,” amesema Aweso.
Awali, Makalla amesema anaifahamu vyema changamoto ya maji wilayani Longido, hata hivyo, amesema kazi kubwa imefanyika ya kutoa maji katika Mto Simba mkoani Kilimanjaro kuyapeleka wilayani humo.
“Nimewahi kuja hapa nikiwa naibu waziri wa maji kazi nzuri ilifanyika, lakini maji hayakutosheleza kuyapeleka Namanga ndiyo maana ulifanyika utafiti wa kupata chanzo cha maji kule Sinya kitakachozalisha maji ya uhakika,” amesema Makalla.