Mbunge CCM ahoji matumizi ya nguvu kusaka watumiaji wa mkaa, Serikali yamjibu.

Dodoma. Mbunge wa Kibamba (CCM), Issa Mtemvu amesema ingawa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ni wa miaka 10, lakini sasa kumekuwa na utumiaji wa nguvu za kutafuta Mtanzania mmoja mmoja anayetumia mkaa katika makazi yao.

Akiuliza swali bungeni leo Alhamisi Septemba 5, 2024, Mtemvu amesema mkakati huo ni wa miaka 10 lakini hivi sasa kumekuwa na utumiaji wa nguvu ya kutafuta Watanzania mmoja mmoja ambao wanatumia mkaa katika makazi.

“Kuna kauli ipi ya Serikali juu ya jambo hili kwa sababu muda bado ni mwingi sana ambao tunaelekea hadi mwaka 2034,” amehoji Mtemvu.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Dk Ashatu Kijaji amesema siyo sahihi kumfuata Mtanzania mmoja mmoja kuangalia ana mkaa ama hana mkaa.

“Kwa sababu kinachofanyika ni kurudi katika misitu yetu, tunazo taasisi zetu zinazosimamia misitu yetu ili iweze kukatwa miti. Kwa sababu ukimfuata Mtanzania mmoja mmoja ndani ya nyumba yake huwezi kujua kama mkaa alionao kama unakibali ama hauna,” amesema.

Amewaomba wenzake ndani ya Serikali kurejea katika masharti na kanuni  zinavyowaelekeza ili waweze kulinda mazingira ya nchi.

“Lakini tuendelee kuelisha wananchi wetu juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema Dk Kijaji.

Katika swali la msingi, Mtemvu amehoji ni mkakati mahsusi wa Serikali wa kukabiliana na matumizi ya mkaa na kuni nchini ili kulinda mazingira.

Akijibu swali hilo, Dk Kijaji amesema Serikali imeandaa na inatekeleza mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) ambao unatoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Mkakati huu unalenga kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” amesema.

Amesema vilevile, mkakati huu unalenga kupunguza gharama za nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia, kuimarisha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uhakika ya nishati safi ya kupikia.

Nyingine ni kuhamasisha uwekezaji katika nishati safi ya kupikia pamoja na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Related Posts