Mchuano uchaguzi Chadema Kanda ya Pwani, Boni Yai arejesha fomu

Dar es Salaam. Dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu kuwania uongozi wa Kanda ya Pwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limefungwa, huku wagombea wawili wa uenyekiti wakioneshana umwamba dhidi ya mwenzake.

Leo Alhamisi, Septemba 5, 2024 saa 10:00 jioni, ndio dirisha limefungwa baada ya kufunguliwa kuanzia Agosti 23, 2024. Waliochukua na kurejesha ni Boniface Jacob maarufu Boni Yai na Gerva Lyenda.

Mbali na hao, wanaowania nafasi za Makamu Mwenyekiti napo wako watiania wawili Shekh Ally Mohamed, maarufu Kadogoo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Pwani, Baraka Musa.

Baada ya dirisha kufungwa, Mwananchi limezungumza na Kaimu Katibu wa Kanda ya Pwani, Jerry Kerenge amesema jumla ya wanachama 32 waliochukua fomu kuwania nafasi mbalimbali na wamesharejesha fomu.

Kerenge amesema nafasi ya mwenyekiti waliochukua na kurejesha fomu ni wawili, sawa na makamu mwenyewe.

“Baada ya kukamilisha hatua hii tunangoja kamati kuu iweze kuwaita kwa ajili ya usahili na hatimaye uchaguzi. Wito wangu kwa watia nia bado hawajawa wagombea, wasubiri kuteuliwa ili waingie kwenye kampeni,” amesema.

Licha ya kutokufafanua zaidi, lakini baadhi ya nafasi zinazowaniwa ngazi ya kanda ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti na mhazini. Pia, kuna nafasi ya wenyeviti na makamu wenyeviti wa mabaraza ya wazee, vijana (Bavicha) na wanawake (Bawacha).

Mchuano mkali unatarajiwa kushuhudiwa kati ya Boniface aliyewahi kuwa Meya wa Ubungo dhidi ya Lyenda ambaye ni Ofisa Habari wa chama wa kanda hiyo.

Wawili hao wamerudisha fomu kwa nyakati tofauti na kila mmoja akieleza kipaumbele chake kuwaunganisha wanachama kuhakikisha wanashinda uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

Pamoja na kwamba ni vigumu kutabiri nani anaweza kushinda katika kiny’ang’anyiro hicho katika nafasi ya uenyekiti lakini Boniface anaonekana kupigiwa chapuo zaidi na wafuasi wengi wanaoonekana kumuunga mkono wakati anarejesha fomu.

Wawili hao wanataka kugombea nafasi hiyo ya uenyekiti ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikikaimiwa na Baraka Mwago na Katibu wa Kanda alikuwa Hemed Ally ambaye alirejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwago alikuwa anakaimu nafasi hiyo kufuatia aliyekuwa anakalia kiti hicho Fredrick Sumaye kushindwa kutetea katika uchaguzi uliofanyika Novemba 28, 2019 Kibaha mkoani Pwani, baada ya kupigiwa kura ya hapana na wajumbe. Hatua hiyo aliilalamikia na mwisho wa siku alirejea CCM.

Sumaye aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa mwongo mmoja kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 alijikuta katika hali hiyo pamoja na kwamba katika uchaguzi huo alikuwa mgombea pekee katika nafasi hiyo.

Umwamba wa Boniface, Lyenda

Leo Alhamisi, Septemba 5, 2024, Jacob amerejesha fomu kwa aina yake. Amesindikizwa na wanachama wa chama hicho kutoka Manzeshe hadi ofisi za Chadema, Kinondoni.

Baada ya kukaibidhi fomu zake, akapata wasaa wa kuzungumza na wafuasi waliomsindikiza akisema Pwani inarejea kwa kishindo huku akitaja sifa tatu za kiongozi anayetakiwa kuiongoza Pwani ili kuhakikisha wanashinda majimbo yote.

“Kiongozi lazima awe na sifa kuu tatu ikiwemo kuaminika, kusikilizwa na kuwa mstari wa mbele kuongoza wananchi, kwakuwa mmenisikiliza na naona mko tayari niwaongoze kwenye mapambano katika Kanda hii ya Pwani,” amesema.

Boniface amesema wanaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wanahitaji kushinda mitaa na kata zote huku akieleza kazi hiyo ni nzito na si nyepesi.

“Mkinipa nafasi hiyo nitakuwa mstari wa mbele kukabiliana na hatari zozote ili kulinda chama chetu. Kitendo cha kuungana hivi wanachama wapaswa kujua tunaanza upya kushikamana kwa kuondoa tofauti zetu,” amesema.

Amesema iwapo atashinda nafasi hiyo katika uchaguzi huo hata kuwa kiongozi wa kujifungia ndani bali atakuwa anafanya ziara maeneo mbalimbali na hata hakishindwa hawezi kulialia.

“Hatakama nikishindwa sitabwatuka bwatuka kupiga kelele ovyo kwa sababu tu nimekosa nafasi ya uongozi sitaenda CCM, nitachukulia wakati wangu bado na ukifika nitarejea,” amesema.

Wakati Jacob akieleza hayo, Lyenda alirudisha na wafuasi wachache na baada ya kumalzia akasema kinachomsukuma kugombea nafasi hiyo ni kutatua changamoto zilizopo pamoja na kuunganisha wanachama kuwa kitu kimoja kuelekea kwenye Uchaguzi ujao.

“Nimesomea na kubobea eneo la utawala nimeona ni muda mwafaka kukisaidia chama changu kupitia taaluma niliyosomea, nikipewa ridhaa nitaunganisha wanachama na kuwatengeneza watu kuwa viongozi,” amesema.

Alichokisema Kadogoo, Mussa

Katika hatua nyingine wanaowania nafasi za Makamu Mwenyekiti wapo watia nia wawili  akiwemo Shekh Ally Mohamed ‘Kadogoo’ na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kisarawe, Baraka Musa wote walieleza yao.

Kadogoo amesema kusindikizwa na umati mkubwa anajiona anadeni kubwa la kulipa wananchama iwapo atashinda baada ya kufanyika uchaguzi.

“Mmetuheshimisha, mmetusindikiza toka maeneo ya Sinza hadi hapa najiona ninadeni kubwa la kuwalipa iwapo nitashinda,” amesema.

Kwa upande wake, Baraka Musa amesema uzoefu alioupata wa kugombea nafasi mbalimbali kukitumikia chama hicho ni wakati sasa wa kwenda kutoa mchango wake ngazi ya kanda.

“Chadema tunaamini kwenye nguzo nne, uhuru na nimeutumia kwa mujibu ya Katiba ya Chadema na tunaamini katika haki nahii ni fursa kwangu lakini tunaamini katika demokrasia ili kuonesha kwa umma hivyo vyote nimechukua fomu kugombea kutekeleza wajibu wangu,” amesema. 

Musa amesema nguzo ya mwisho ni maendeleo alianza tangu akiwa kiongozi wa Baraza la Vijana (Bavicha), huku akieleza anadhamira ya kweli katika kuongoza.

“Sitaki kuongea japo kuna wanaojua kuongea zaidi mitandaoni niwaombe wenzangu tukutane katika midahalo tuone itakuwaje,” amesema.

Mwenyekiti wa Chadema Kawe, Ronald Manyama amesema wanahitaji kiongozi mzoefu na mwenye nguvu katika kuongoza kanda ya Pwani kwakuwa inatoa taswira ya Chama hicho kitaifa.

“Tumewai kuongoza Jiji la Dar es Salaam kwa kuchaguliwa na wananchi bila kuhitaji mbeleko tumeongoza kawe,Ubungo, kibamba na Ukonga tumeongoza kwa sababu kuchaguliwa kwa mapenzi ya wananchi na tunajipanga kupata mgombea anayekubalika,” amesema.

Katika maelezo yake, Manyama amesema katika wagombea waliojitokeza Boniface anastahili kwakuwa na sifa anazoona zinafaha katika kuongoza kanda hiyo kwa kuzingatia hatua na nafasi alizowai kushika.

“Hata wapinzani wanatambua mtu hatari kwao ni Boniface amekuwa tishio kwao ndiyo maana unaona kunahujuma zinaendela kutaka asigombee nafasi hii,” amesema Manyama.

Mwenyekiti wa Chadema Kibamba, Erenest Mgawe amesema wanahitaji kupata kiongozi bora wa kuwavusha katika chaguzi zilizombele na kuhakikisha wanachukua viti vingi.

“Tunatakiwa kupata kiongozi mwenye msimamo na anayekijua chama lakini kwakuwa wanachama tuona na tunawajua ni jukumu letu katika kipindi hiki kuangalia,” amesema.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts