Unguja. Wakati kukiwa na harakati za kuweka mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu, imeelezwa sera na sheria zinasozimamia kundi hilo zina upungufu hivyo ipo haja ya kuziangalia namna zinavyowajumuisha.
Hayo yamebainika wakati wa mkutano wa programu ya kimataifa ya haki za watu wenye ulemavu uliofanyika Mjini Unguja ukilenga kushughulikia changamoto zinazowakabili.
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeida Rashid Abdallah amesema miongozo na sera inayohusu watu wenye ulemavu kwa sasa haitoshelezi.
“Sera ya mwaka 2004 inayohusu watu wenye ulemavu haitoshelezi hivyo ipo haja ya kuangalia sera na sheria zingine namna ilivyowajumuisha watu hawa ili kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma,” amesema.
Amesema kukosekana masilahi muhimu katika vitu hivyo, wanalazimika kupaza sauti kuieleza jamii changamoto zinazowakabili kutokana na upungufu uliopo kwenya sera na sheria iliyopo.
Amesema pale unapoonekana upungufu lazima waonyeshe na nini kinahitajika kufanyika.
Hata hivyo, Abeida amesema muda si mrefu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itazindua mpangokazi wa kitaifa wa kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao umezingatia masuala ya watu wenye ulemavu.
Ili kutekeleza mambo hayo kwa usawa, amesema ingawa Serikali inaweza kuweka takwimu zao lakini ni vyema hata wao wenyewe wakawa na takwimu zinazowahusu jambo litakalowasaidia wakati wa kutoa maoni.
Mtaalamu wa ushauri wa masuala ya usawa wa kijinsia, Maja Hansen amesema mkutano huo wa haki za watu wenye ulemavu umelenga kuzungmzia ajenda nne zikiwamo ushiriki na ushirikishaji, na ulinzi wa vitendo vya ukatili kwa watu wenye ulemavu.
Mengine ni kuangalia maboresho ya sera na masuala ya takwimu.
Ali Omar Makame kutoka Shirikisho la Jumuiya la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (Shijuwaza), amesema watahakikisha wanashiriki kutoa maoni ili kubadilisha mambo wanayoona hayapo sawa katika kundi hilo.
Moja ya changamoto alizoeleza zinawakabili watu wenye ulemavu ni ukosefu wa vyoo rafiki kwa baadhi ya majengo ya Serikali na binafsi.