Mkutano wa Focac utakavyoimarisha uchumi wa Tanzania, Afrika

Marais karibu wote wa nchi za Afrika hivi sasa wako nchini China katika mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), ambao umeanza jana na unatarajiwa kuhitimishwa kesho.

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo uliotanguliwa na kikao cha mawaziri wa mambo ya nje ni Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye aliwasili katika Taifa hilo la pili kwa uchumi duniani siku mbili kabla ya mkutano kuanza.

Aidha tangu kuanza kwake mwaka 2000, FOCAC imewezesha miradi mikubwa ya miundombinu barani Afrika, kama vile ujenzi wa barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari pamoja na uwekezaji katika nishati.

Ushirikiano chini ya FOCAC umeongeza biashara kati ya Afrika na China, huku nchi za Afrika zikipata soko kubwa kwa bidhaa zao za kilimo, madini na malighafi nyingine, na kunufaika na uagizaji wa bidhaa za bei nafuu kutoka China.

Mkutano wa mwaka huu unatarajia kuimarisha ambayo tayari yamekuwa yakifanyika na zaidi kuongeza mambo mapya muhimu kati ya Taifa hilo kubwa linaloendelea na bara lenye mataifa mengi yanayoendelea.

Balozi wa Tanzania nchini China, Khamis Omar anasema Focac mwaka huu ni ya kuendeleza pale ilipoishia Focac ya mwaka 2021, hivyo kuna matarajio ya manufaa zaidi kuliko kipindi kilichopita.

Akizungumza na Shirika la habari la CGTN wakati wa mkutano huo, Balozi Omar anasema mkutano huu unaimarisha uhusiano mkubwa wa kiuchumi uliopo kati ya Tanzania na China, akitolea mfano eneo la miundombinu.

“Binafsi natazama maeneo makuu matatu au manne muhimu. Kwanza ni kwenye maendeleo ya miundombinu, wakati tunapozungumzia China na Tanzania, jambo la kwanza linalokuja akilini kwa watu wazee kama mimi ni reli ya Tazara. Hii ilikuwa mwanzo wa ushirikiano mkubwa wa miundombinu,” anasema.

Anaongeza kuwa kila mtu anajua miundombinu ni muhimu sana kwa kufungua uchumi wa nchi yoyote, kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko, na kuunganisha nchi na dunia nzima.

“Eneo la pili ni upande wa uzalishaji, China, hata wakati wa miaka ya 1960 hadi sasa, imekuwa ikiunga mkono Tanzania katika maeneo ya uzalishaji, kilimo, na viwanda. Sasa pia kuna nguvu ya sekta binafsi pande zote mbili. China imekuwa mshirika wetu mkuu wa kibiashara, nafikiri kwa miaka minane au tisa iliyopita,” anasema.

Balozi Omar alisisitiza kuwa China ni namba moja kama mshirika wa kibiashara na kama tunavyojua, biashara ni muhimu sana kwa ukuaji. Utalii, kama ulivyosema, pia tunauona ukikua.”

Mchambuzi mwandamizi wa uchumi, Profesa Haji Semboja anasema hivi sasa China imepiga hatua kubwa katika teknolojia, hivyo kuimarisha uhusiano nao kupitia jukwaa hilo kunaweza kufanikisha mipango wa maendeleo.

“China sasa wapo mbele kwa teknolojia kuliko wengi, imepiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda, hivyo sasa wanaangalia washirika wa kibiashara. Mkutano kama huu unatoa fursa ya kuvuta uwekezaji na soko la kuuza rasilimali zetu,” anasema Profesa Semboja.

Anasema ni muhimu kwa Tanzania kushiriki, kwani endapo ikikaa nyuma inakuwa haipo kwenye mipango yao hivyo hata manufaa yanaweza yasipatikane.

“Muhimu tusifikiri kuwa fursa tu zitakuja kwa kuwa tuna mahusiano nao mazuri, ni lazima tuweke mazingira ya kuvutia uwekezaji, uzuri ni kwamba sasa hivi wao wana uwezo mkubwa sekta muhimu na Serikali inawaunga mkono,” anasema.

Wachambuzi wengine wanaamini kuwa kupitia miradi ambayo itapatikana baada ya Focac itasaidia kupunguza ukosefu wa ajira, kuongeza kipato cha kaya, na kuboresha hali ya maisha.

Miradi ya kilimo barani Afrika ambayo inatarajia kutoka na Focac inatarajia kuongeza ufadhili wa sekta hiyo katika umwagiliaji, mafunzo ya kilimo bora, na utafiti wa kilimo. Hii imeongeza tija ya kilimo, kupunguza umaskini, na kuimarisha usalama wa chakula.

Mwanazuoni wa sera za Afrika, Profesa Peter Kagwanja anasema FOCAC imekuwa jukwaa muhimu la ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika, likichangia ukuaji wa uchumi, maendeleo ya miundombinu, na kuboresha ustawi wa jamii barani Afrika.

Anasema FOCAC ni lango la Afrika kuelekea kwenye Mpango wa Ukanda na Njia (BRI), mradi wa kunufaika na mabilioni ya dola wa China. Kwa kipindi cha miaka 24 iliyopita, kupitia FOCAC na BRI, China imeelekeza zaidi ya dola bilioni 200 kusaidia maendeleo ya bara la Afrika.

Anasema siku zote China inaunga mkono Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063, mpango wa maendeleo ya Afrika. Matokeo yake ni kwamba Afrika sio tena bara lisilo na matumaini, bali ni mpaka mpya wa ukuaji imara.

Mwalimu huyo wa vyuo kadhaa nchini Kenya anasema: “China ni mshirika mkuu wa kibiashara wa Kenya. China inaweza kuongeza uwekezaji katika uundaji wa viwanda, ukuzaji wa uwezo, na mafunzo ya kiufundi ili kusaidia vijana kupata ajira katika masoko ya ajira ya ndani na ya kimataifa.

“Kenya ni moja ya nchi 52 kati ya nchi 54 za Afrika zinazoshiriki katika mpango huu. Mkutano wa FOCAC 2024 unatoa fursa nzuri kwa China na Kenya kuboresha uhusiano wao kwa viwango vipya kabisa,” anasema.

Taarifa iliyotolewa Agosti 31, 2024 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ilieleza kuwa Rais Samia anatarajiwa kuwasilisha miradi minne kwa Serikali ya China kwa lengo la kupatiwa fedha za mkopo nafuu na msaada ya utekelezaji wake.

Miradi ambayo Waziri alisema itakayowasilishwa na Rais Samia kwenye mkutano huo ni ujenzi wa mtandao wa mawasiliano vijijini awamu ya pili, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 awamu ya pili na ya tatu, ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (Veta) awamu ya pili na ujenzi wa barabara za Zanzibar zenye urefu wa kilomita 277.

“Tanzania inatarajia kuwasilisha miradi mbalimbali, ikiwemo mipya na ile ambayo haikuweza kutekelezwa kwenye mpango uliopita wa FOCAC kwa sababu mbalimbali, ili iweze kupatiwa fedha za mkopo nafuu na msaada na kutekelezwa chini ya mpango kazi wa FOCAC mwaka 2025-2027,” amesema.

Balozi Kombo anataja malengo matatu ya Tanzania kushiriki mkutano huo; mosi ni kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China ambao mwaka huu umetimiza miaka 60.

Jambo la pili ni kujadiliana na kukubaliana na Serikali ya China namna ya kuendelea kuongeza ushirikiano katika maeneo ya kipaumbele kama sekta ya miundombinu, mifumo ya chakula, biashara na uwekezaji, kubadilishana ujuzi, upatikanaji wa nishati safi na salama na kusaidia ujenzi wa uchumi wa kidijitali.

“Pia kuibua fursa mpya za ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili, kutangaza maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika sheria za sekta ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi,” anasema.

Balozi Kombo alisema Rais Samia atafanya mazungumzo na kampuni za China ambazo zipo tayari kufanya uwekezaji mkubwa na kufungua ofisi zao nchini Tanzania.

“Atakutana na kampuni kubwa za China kwa pamoja katika hafla ya chakula cha jioni, yenye lengo la kuhamasisha kufanya uwekezaji nchini Tanzania,” alisema.

Akiwa China, Rais Samia atafanya mkutano na Rais Xi Jinping kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.

Kwa mujibu wa Ikulu, wakati wa ziara hiyo katika kukuza biashara na uwekezaji, Rais Samia atakutana na makampuni na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji zaidi nchini Tanzania.

Related Posts