Mpole, Okutu wapewa akili mpya Pamba Jiji

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Pamba, Stand United na Mbeya City, Abasirim Chidiebere raia wa Nigeria amesema mwanzo mgumu iliyoanza nao Pamba Jiji katika Ligi Kuu Bara ni kutokana na udhaifu wa eneo la ushambuliaji na kiungo, huku akiwataka mashabiki kutuliza presha.

Chidiebere aliyestaafu soka na ameweka makazi jijini Mwanza, aliliambia Mwanaspoti Pamba Jiji imefanya usajili mzuri, lakini inakwamishwa na umaliziaji kutokana na mshambuliaji kinara, George Mpole kukosa ubora aliokuwa nao misimu miwili iliyopita akimaliza kinara wa mabao.

Mnigeria huyo alisema Pamba inakwamishwa pia na kukosa ubora katika eneo la kiungo ambacho kinaweza kutengeneza nafasi za mabao kwa washambuliaji na kuamua mechi, huku akishauri benchi la ufundi kumtumia mshambuliaji Mghana, Erick Okutu nyuma ya straika badala ya kuwa kinara wa eneo hilo.

“Haya ni mapito tu, lakini naamini Pamba itafanya vizuri mimi sina mashaka kabisa na hii timu, nafahamu wachezaji na kocha wako kwenye presha kubwa na wana Mwanza wana hamu wanatamani timu ishinde hivyo kuna presha kubwa ikizingatiwa kwamba ina miaka zaidi ya 20 haiko Ligi Kuu,”€ alisema Chidiebere

Mshambuliaji huyo aliwataka mashabiki kuwa na imani na timu yao, kuiunga mkono na kuipa nguvu ya kuendelea kupambana badala ya kuwapa presha wachezaji na benchi la ufundi kutokana na matokeo ya michezo miwili ya Ligi Kuu.

“Usajili wao ni mzuri wamemleta George Mpole nadhani bado anakosa ule uzoefu wa Ligi yetu kwa sababu ushindani umeongezeka tofauti na alivyokuwepo. Hatutaki vitu vya kubahatisha.”

Related Posts