Mwanariadha Rebecca Cheptegei amefariki siku chache baada ya kumwagiwa petroli na kuchomwa moto na mpenzi wake wa zamani. Mwanariadha huyo wa mbio za marathon wa Uganda mwenye umri wa miaka 33, alikuwa ameshiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Paris ya hivi majuzi.
Ripoti iliyowasilishwa kwa maafisa wa polisi inaarifu kuwa mwanariadha huyo na mpenzi wake wa zamani walikuwa wakizozana kuhusu kipande cha ardhi, na kwamba alishambuliwa baada ya kurejea nyumbani kutoka kanisani siku ya Jumapili.
Daktari Owen Minach kaimu afisa msimamizi katika hospitali ya rufaa ya Moi jijini Eldoret amesema mwanariadha huyo alipata majeraha ya moto yaliyouchoma mwili wake kwa zaidi ya asilimia 80.
“Kawaida wakati ngozi imeathirika kwa kiwango hicho, tunampa mgonjwa dawa aina ya antibiotiki ya kutosha na dawa nyingine na kutumia teknolojia nyingine kwa lengo kuu la kulinda mwili kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa viungo vyake .”
Waziri wa michezo Kenya aahidi haki
Shirikisho la riadha la Uganda limelaani tukio hilo la unyanyasaji wa kijinsia na wamezitaka asasi za kiusalama kuhakikisha mwanariadha huyo amepata haki.
Waziri wa michezo wa Kenya Kipchumba Murkomen ameeleza kupitia taarifa kwa vyombo vya habari kuwa kifo cha Rebecca ni pigo kubwa sio tu kwa taifa la Uganda bali kwa kanda nzima ya Afrika mashariki.
Soma pia: Olimpiki Paris 2024: Wanariadha wa Afrika wang´ara
Amesema tukio hili limemulika haja ya kukabiliana vikali na dhuluma za kijinsia huku akiahidi kwamba Kenya itahakikisha haki imepatikana.
Baba wa mwanariadha huyo, Joseph Cheptegei amesema wamempoteza mtu pekee aliyekuwa tegemeo lao maishani. Ameikosoa serikali kwa utepetevu katika kulishughulikia tukio hilo.
Rebecca ni mmoja tu wa wanariadha kadhaa wasomi waliouawa nchini Kenya na watu waliokuwa na uhusiano nao.
Mnamo Oktoba 2021 Polisi nchini Kenya walimkamata mume wa mwanariadha wa masafa marefu aliyevunja rekodi Agnes Tirop ambaye aliuawa kwa kuchomwa kisu nyumbani kwake.
Mnamo Aprili 2022 Polisi walianzisha msako wa kumtafuta mpenzi wa Ethiopia Damaris Muthee Mutua, 28, ambaye alizaliwa nchini Kenya lakini alikuwa akiiwakilisha Bahrain, ambaye mwili wake ulipatikana katika mji wa Iten, mji maarufu kwa wakimbiaji wa masafa marefu.