Rais Macron amteua Michel Barnier kuwa Waziri Mkuu mpya – DW – 05.09.2024

Michel Barnier, aliyewahi kuwa mpatanishi wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo ya Brexit, anateuliwa na Rais Macron katikati ya sintofahamu ya kisiasa nchini humo, na ambaye anakabiliwa na jukumu zito la kuiunganisha serikali. Barnier mwenye miaka 73, anakuwa waziri mkuu mwenye umri mkubwa kabisa kuteuliwa katika historia ya sasa nchini humo, tofauti na mtangulizi wake Gabriel Attal, aliyekuwa na miaka 35.

Uteuzi wa mwanasiasa huyu mkongwe, na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ufaransa, anayetokea chama cha mrengo mkali wa kulia cha Republicans, LR na asiyefungamana na mrengo wa Macron wa siasa za wastani, umepokelewa kwa fadhaa na mrengo wa kushoto, wenye idadi kubwa ya viti bungeni na ambao unaweza kumuangusha kwa kura ya kutokuwa na imani naye.

Kihunzi kingine atakachokumbana nacho bungeni ni makundi makubwa mawili ya kisiasa, la kwanza likiwa ni lile la Macron na la siasa za mrengo mkali wa kulia la National Rally, linaloongozwa na Marine Le Pen. 

Soma pia:Macron aongeza juhudi za kuvunja mkwamo wa kisiasa

Melenchon aahidi kuihamasisha nguvu ya umma kupinga uteuzi wa Barnier

Kiongozi wa chama cha LFI cha mrengo mkali wa kushoto Jean Luc-Melenchon ameukosoa vikali uteuzi huo, akisema Macron anataka kuunda serikali ambayo haitaakisi matakwa ya watu wa Ufaransa na kuamua kuungana na mrengo wa kulia, huku akipuuzilia mbali matokeo ya uchaguzi.

Uchaguzi wa gunge, Ufaransa
Kiongozi wa chama cha mrengo mkali wa kushoto Jean Luc-Melenchon amesisitiza kwamba Rais Emmanuel Macron hakuzingatia matakwa ya watu alipomchagu waziri mkuu Michel BarnierPicha: Thomas Padilla/AP/dpa/picture alliance

“Rais wa Jamhuri amemteua Waziri Mkuu. Ni Mheshimiwa Michel Barnier. Majibu yetu, hayatahoji sifa zake kama binaadamu. Hilo si suala la msingi. Mbali na hayo, Rais ameamua kuyakataa rasmi matokeo ya uchaguzi wa wabunge aliouitisha yeye mwenyewe.”

Ni kwa hatua hiyo, Melenchon amesema atawahamasisha watu kuandamana Septemba 7, kwa jina la kuheshimu demokrasia, heshima kwa taasisi za jamhuri, zilizo chini ya mamlaka ya watu na kwa ajili ya utu binafsi wa wapiga kura.

Soma pia:Macron aondoa uwezekano wa kuteua waziri mkuu kutoka mrengo wa kushoto

Marine Le Pen, anayeongoza chama cha National Rally amesema tu kwamba chama chake kinasubiri kusikia mipango ya Barnier kabla ya kuamua kumuunga mkono ama la. Kiongozi huyu mpya anatarajiwa kuweka wazi mipango yake katika hotuba ya kwanza bungeni.

Barnier, hakuonekana popote katika uwanja wa siasa nchini Ufaransa tangu aliposhindwa kwenye uteuzi wa chama wa kugombea urais mwaka 2022, ambapo alipigia debe suala la kuwazuia wahamiaji.

Waziri mmoja wa serikali inayoondoka madarakani ambaye hakutajwa kutambulishwa, amemuelezea Barnier kuwa anayependwa sana na wabunge wa mrengo wa kulia, lakini pia asiye na chuki na mrengo wa kushoto.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen ameukaribisha uteuzi huo na kuandika kwenye ukurasa wa X kwamba anaamini Barnier atayatekeleza kwa uzito mkubwa majukumu yake kwa kuzingatia maslahi na Ulaya na Ufaransa, kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu na kumtakia majukumu mema.

Waziri Mkuu wa kwanza wa Macron, Edouardo Philipe pia amempongea kiongozi huyo mpya, sanjari na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani.

Related Posts