Rais Samia mgeni rasmi Baraza la Maulid Geita

Geita. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Baraza la Maulid linalotarajiwa kufanyika kitaifa mkoani Geita, Septemba 16, 2024.

Shekhe wa Mkoa wa Geita, Alihaji Yusuph Kabaju amebainisha hayo leo Septemba 5, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sherehe ya Maulid zinazotarajiwa kufanyika kitaifa mkoani humo.

Amesema Baraza la Maulid litatanguliwa na sherehe za Maulid ambazo zitaongozwa na Shekhe Mkuu na Mufti wa Tanzania, Abubakar Zuber na zinatarajiwa kufanyika kwenye viwanja vya Kalangalala mjini Geita.

“Maulid haya yatatanguliwa na wiki ya Maulidi itakayoanza Septemba saba na itaambatana na shughuli mbalimbali za kijamii, pia, tutajadili mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya ya ukatili wa kijinsia yaliyokithiri kwa wingi na sisi kama viongozi wadini tunaendelea kukemea kwakuwa matukio haya hayampendezi Mwenyezi Mungu,” amesema Kabaju.

Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Mkoa wa Geita (Bakwata), Abas Mtunguja amesema wiki ya sherehe za maulidi zitatanguliwa na matukio mbalimbali ikiwemo mashindano ya mpira wa miguu, maonyesho ya wafanyabiashara pamoja na  makongamano ya siku tatu yakihusisha makundi ya viongozi wa dini, vijana na wanawake.

Amesema Shekhe Mkuu anaetarajiwa kuingia mkoani Geita Septemba 12 na atatembelea kaburi la Hayati John Magufuli kisha kwenda wilayani Bukombe kuzindua msikiti uliojengwa na Naibu Waziri Mkuu, na Waziri wa Nishati, Doto Biteko.

Shekhe Zuberi pia atakuwa na kikao na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella kisha Septemba 14 atatembelea mgodi wa dhahabu wa Geita na badaye kufunga mashindano ya mpira.

Mtunguja amesema katika wiki hiyo ya Maulid kutakuw ana maonyesho ya elimu ya dini na kufuatiwa na maandamano ya vijana kabla ya kufanyika kwa Maulid ya Kitaifa itakayoanza saa moja jioni Septemba 15, 2024

Related Posts