WAKATI timu tano zikipambana kujinasua zisishuke daraja katika ligi ya kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BD), baadhi ya makocha wa timu hizo wamesema kwa sasa walipofikia ni kuombeana mabaya.
Timu hizo ni KIUT, Jogoo, Ukonga Kings, Mgulani JKT, huku timu tatu ndizo zinatakiwa kushuka daraja.
Wakiongea kwa nyakati tofauti na Mwanaspoti makocha hao walisema wanatarajia kuona ushindani ukiongezeka katika kipindi hiki.
Kocha Abbas Sanawe kutoka Crows alisema bila ya kupambana unaweza ukashuka daraja akitolea mfano timu yake ambayo alisema haipo katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi.
“Kujinasua kwetu tunatakiwa tushinde michezo mitano iliyobaki na huku sisi tukiombea timu nyingine zipoteze michezo yao,” alisema Sanawe.
Alisema licha ya timu hizo tatu kuwa na viwango vizuri, kwa upande wao mkakati waliopanga ni kushinda michezo yote mitano.
Akizidi kuelezea alisema pamoja na kushika nafasi ya 14 kwa pointi 29 katika msimamo wa ligi, timu yake ina uwezo wa kushika hadi nafasi ya 11.
“Kushika nafasi hiyo itategemea kushinda michezo iliyobakia, itakayotufanya tuwe na pointi 39,” alisema Sanawe.