Serikali kuja ya utaratibu mpya wanaoomba nafasi za kujitolea

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema mwongozo wa kujitolea katika utumishi utakamilika ndani ya mwaka wa fedha 2024/25.

Mbali na hilo, Serikali imesema itaweka utaratibu wa ushindani ili kijana aende kujitolea sehemu kama inavyofanyika kwa nafasi za ajira.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 5, 2024 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Tendega.

Grace amesema wamekuwa wakiona taasisi mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zinawapa vijana nafasi za kujitolea, lakini hakuna utaratibu maalumu uliowekwa wa kujua wanapata kwa namna gani, nafasi hizo.

“Hii inaweza kutokea ama bosi ama mfanyakazi akaweza kumpatia nafasi hiyo. Matokeo yake tunavyokuwa tunaomba vijana hawa wapatiwe ajira kwa sababu wamejitolea unakuta unaweka mlolongo wa walewale ambao wamewekwa katika mfumo huo,” amesema.

Amehoji nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kunakuwa na utaratibu maalumu wa kuwapata vijana wanaojitolea katika taasisi mbalimbali za umma.

Pia, amehoji ni lini mwongozo wa utaratibu kuchukua vijana wa kujitolea utatolewa.

Akijibu swali hilo, Sangu amesema Serikali baada ya kuona changamoto ya namna ya kuwapata vijana wa kujitolea, iko mbioni kuandaa randama ambayo baada ya kukamilika, watatoa waraka wa namna ya utaratibu wa kuwapata vijana hao utakavyokuwa.

“Kwa namna ya pekee Serikali imeona, itaweka utaratibu wa ushindani ili kijana aende kujitolea sehemu. Tunakwenda kuweka utaratibu kama tunavyofanya kwenye ajira za sasa ambazo zimetangazwa kwenye kada ya elimu, afya na nyingine,” amesema.

Kuhusu lini mwongozo utakamilika, Sangu amesema kabla ya kukamilika kwa mwaka huu wa fedha 2024/25, waraka huo utakuwa umetoka kwa ajili ya kuwaongoza wakuu wa taasisi namna ya kuwapata vijana wa kujitolea.

Katika swali la msingi Grace amehoji ni kwa nini Serikali isiwalipe posho sawa ya kujikimu wafanyakazi wanaojitolea ili kuondoa matabaka ya malipo kulingana na sehemu wanazofanya kazi.

Akijibu swali hilo, Sangu amesema Serikali inaruhusu waajiri mbalimbali katika utumishi wa umma kuwatumia wahitimu wa vyuo katika ngazi mbalimbali za elimu kufanya kazi kwa kujitolea katika maeneo yao ya kazi ili kupata uzoefu wa kazi kwa fani zao.

“Kwa kuwa wahitimu hao siyo watumishi wa umma, miongozo ya kiutumishi haijaelekeza utaratibu wa kuwalipa mishahara au posho ya kujikimu,” amesema. 

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa wafanyakazi wanaojitolea katika utumishi wa umma.

Sangu amesema katika kuhakikisha matumizi sahihi ya wafanyakazi wa kujitolea, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mwongozo wa kujitolea katika utumishi wa umma.

Amesema mwongozo huo utaweka utaratibu kwa waajiri au sekta na kada mbalimbali wa namna ya kuwapata, kuwasimamia na kuwalipa masilahi wafanyakazi watakaojitolea katika taasisi zao.

Related Posts