Dar es Salaam. Baada ya kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa makandarasi mbalimbali juu ya kucheleweshwa kwa malipo yao, Serikali imesema imeanza mazungumzo na taasisi za kifedha ili kuagalia namna ya kuwasaidia ikiwemo kupunguza madeni inayodaiwa.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Septemba 5, 2024 na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alipokuwa akihutubia katika maadhimisho ya siku ya wahandisi yaliyoandaliwa na Bodi ya Usajili ya Wahandisi Tanzania (ERB) uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Pia kauli hii ya Bashungwa inakuja ikiwa ni siku sita tangu Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko akizungumza bungeni jijini Dodoma, ambapo aliomba mwongozo wa Spika akitaka makandarasi wa ndani kulipwa kwa wakati au kulipwa riba pale malipo yao yanapochelewa, kama ilivyo kwa wale wa kigeni.
Akizungumza katika mkutano huo, Bashungwa amesema anafahamu kuwa kuna changamoto ya mtiririko wa fedha (cashflow) kwa upande wa makandarasi.
“Sisi upande wa Serikali tunaendelea kujipanga kupitia Wizara ya Fedha kuhakikisha tunapunguza madeni lakini tunakaa na mabenki kuangalia namna ambayo wao wakijua kilichopo na kile mnachotudai waweze kuwapa ahueni kidogo katika malipo,” amesema.
Amesema Jana Septemba 4 alikaa na benki ya NMB na kuzungumza nao na baadaye leo atakaa na benki CRDB ili kuangalia namna ya kuwasaidia makandarasi.
“Lakini dhamira ya Serikali kutowaacha peke yenu, tutaendelea kukaa kuangalia namna ya kushirikiana pamoja ili fursa zinazotengenezwa kwa dira na maono ya Serikali makandarasi wazawa waweze kunufaika,” amesema.
Akizungumzia suala la malipo, Msajili wa CRB, Rhoben Nkori amesema ni ngumu kuwa na takwimu halisi za madai ya makadarasi kwa sababu wanafanya kazi katika sekta tofauti na wao ndiyo wanapewa hati za malipo.
“Sisi CRB si sehemu ya malipo ila takwimu halisi za madeni haya zinaweza kupatikana Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi au taasisi wanazofanyia kazi,” amesema Nkori.
Waziri Bashungwa alitumia jukwaa hilo pia kurudia kuonyesha kutopendezwa na tabia ya baadhi ya makandarasi ambao ni wababaishaji huku akiitaka CRB kuwashughulikia.
“Nimepata orodha ya makandarasi wanaojenga majengo mikoa mbalimbali, wanasaini mikataba, akipewa malipo ya awali uswahili unaanza, mteja anahangaika anakuja wizarani, CRB mpo. CRB nimewaambia kama sheria ni dhaifu ileteni ili muwe wasimamizi wazuri mnaozingatia viwango vya majengo,” amesema Bashungwa.
Amesema baadhi ya makandarasi hao wamekuwa wakibadilisha hata mifumo ya maisha huku akitolea mfano wa magari.
“Unakuta mtu alikuwa anaendesha gari ya kawaida Carina anasema yeye anataka VXR, hatuwezi kwenda namna hii, kula kwenye mshahara wako usile katika fedha ulizopewa na mteja kwa ajili ya kufanya kazi yake,” amesema Bashungwa na kuongeza
“Hivyo CRB pamoja na hizi fursa tunazotengeneza tunataka msimamie taratibu ili msiharibie, makandarasi wengi wanafanya kazi nzuri hawa wachache wasifanye wateja washindwe kufanya kazi na makandarasi wazawa, tutashughulika nao’.
Akijibia kuhusu ucheleweshaji wa miradi unaofanywa na makandarasi na kuibua malalamiko kutoka kwa wateja, Nkori amesema hatua huwa zinachukuliwa.
Amesema CRB inapopokea malalamiko huyafanyia uchunguzi na endapo mkandarasi akibainika kuwa na makosa ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria ya usajili wa makandarasi na adhabu itaendana na kosa lake.
“Endapo mkandarasi atabainika kufanya makosa hatua itachukuliwa kwa mujibu wa sheria ya usajili wa makandarasi adhabu italingana na makosa anayofanya na inaweza kuwa kutozwa faini, kusitishwa usajili wake kwa muda maalumu au kufutiwa usajili kutokana na makosa aliyoyafanya,” amesema Nkori.
Katika hatua nyingine, Bashungwa amesema kama Serikali inaendelea kutoa fursa kwa makandarasi wazawa ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miundombinu.
Akitolea mfano wa ujenzi wa kilomita 120 za lami zinazotarajiwa kujengwa katika mwaka 2024/2025 amesema zitashindanishwa kwa makandarasi wazawa pekee, huku akibainisha kuwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) imeagizwa izingatie kutumia makandarasi wa ndani.
Mbali na hilo, Bashungwa amesema tayari wamekaa na wadau wa maendeleo kuangalia namna ambavyo wanaweza kubadili mfumo wa manunuzi.
“Kwa sababu miradi mingi wanaotoa fedha manunuzi yanafanyika kwa masharti yao lakini pia wataombwa kama ambavyo ununuzi unafanywa na Tanroads na wao wafanye kulegeza masharti, ili miradi mikubwa iwe na uwezo wa kuweka makandarasi wasaidizi wazawa ili kupunguza asilimia ya miradi mikubwa kwenda kwa makandarasi wa nje,” amesema Bashungwa.
Katika hoja yake Matiko akitumia kanuni ya 76 kuomba mwongozo wa Spika kuhusu utata wa majibu ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipojibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu, Bupe Mwakang’ata.
Mwakang’ata aliuliza swali la nyongeza kwenye swali la msingi namba 66 lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso kuhusu malipo ya makandarasi wazawa.
Mwakang’ata alitaka kujua ni kwa nini makandarasi wa nje wanapocheleweshewa malipo hulipwa na riba, lakini wa ndani wanapocheleweshwa hawalipwi riba.
Matiko alisema: “Waziri wa Fedha anasema wanafanya wanayoyafanya kwa sababu makandarasi wa nje wanapoingia mikataba ya kufanya kazi, wanafuata viwango vya kimataifa, lakini makandarasi wa ndani kwa taratibu zilizopo ndizo zinazowataka hata wakicheleweshewa wasilipwe riba.”