Sure Boy: Kazini kwangu kuzito

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Salum Abubakar ‘Sure Boy,’ ameweka wazi kuwa chini ya kocha Miguel Gamondi, kila mchezaji ndani ya kikosi cha Yanga ana nafasi ya kucheza, mradi aonyeshe juhudi binafsi. Sure Boy, ambaye anacheza nafasi sawa na Mudathir Yahya, Clatous Chama, Stephane Aziz Ki, Duke Abuya na Pacome Zouzoua, alisema ushindani wa namba umekuwa muhimu kwa kuimarisha ubora wa timu na wachezaji wote.

Kiungo huyo wa zamani wa Azam FC, alikiri kuwa licha ya changamoto ya kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, amekuwa akionyesha mabadiliko ya uchezaji na kutumia fursa anapopata nafasi ya kucheza. Alisisitiza, Yanga ina wachezaji wengi wenye uwezo, na kocha Gamondi anatoa nafasi sawa kwa kila mchezaji, huku akizingatia jitihada binafsi na mchango wa kila mmoja.

Akizungumzia ushindani ndani ya kikosi, Sure Boy alisema changamoto ya ubora ipo katika kila eneo, na kwamba mabadiliko makubwa ya uchezaji aliyoyaona tangu alipojiunga na Yanga yamechangiwa na mipango mikubwa na mikakati ya timu hiyo.

Sure Boy alisifu uongozi imara na benchi la ufundi lenye umakini, ambao umewapa nguvu wachezaji kufikia malengo makubwa, hususan katika mashindano ya kimataifa.

Pia ametaja kuwa Yanga ni timu kubwa inayotamani mafanikio makubwa, na jitihada za uongozi na wachezaji zimewezesha timu hiyo kuwa bora, huku malengo yao yakiwa ni kufanikiwa zaidi kimataifa.

“Yanga ni timu kubwa sio tu kwa kuzungumzwa hadi vitendo wachezaji wanatamani kufika mbali kiuchezaji na mafanikio tunaongezwa nguvu na namna viongozi ambavyo wamekuwa wakitoa ushirikiano wa hali na mali kuhakikisha tunafikia mafanikio,” alisema Sure Boy, mtoto wa winga wa zamani wa kimataifa wa Sigara, Yanga na Tanzania Stars, Abubakar Salum ‘Sure Boy Sr na kuongeza;

“Tunafikia malengo makubwa kimataifa jambo ambalo linawezekana kutokana na uwekezaji uliopo kuanzia wachezaji, benchi na uongozi,”aliongeza staa huyo wa zamani wa Azam Fc.

Related Posts