Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali nchini hivi sasa ni za nje ya msimu ambazo zinasababishwa na upepo unaotoka baharini.
Imesema mvua za msimu wa vuli bado hazijaanza na zitaanza mwanzoni mwa Oktoba hadi Desemba 2024 huku zikitarajiwa kuwa za wastani na chini ya wastani.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Septemba 5, 2024, Meneja Utabiri wa TMA, Dk Mafuru Kantamla lililotaka kujua mwenendo wa hali ya hewa amesema mvua zinazonyesha kwa sasa ni za nje ya msimu ambazo zinapita.
“Zinasababishwa na upepo unaotoka Mashariki ambao tunao mpaka sasa unaotoka baharini kuja kwenye maeneo yetu. Upepo huo unachukuwa unyevunyevu ambao upo baharini hivyo kusababisha hizi mvua zinazoendelea ambazo hazimaanishi msimu umeanza,” amesema.
Amesema, msimu wa vuli utaanza mwanzoni mwa Oktoba ingawa amebainisha utakuwa na mvua za kusuasua na za mtawanyiko usioridhisha kutokana na uwepo wa hali ya La-Nina katika eneo la kati la Kitropiki la Bahari ya Pasifiki.
La-Nina ni uwepo wa joto la bahari la chini ya wastani katika eneo la kati la kitropiki la bahari ya Pasifiki
“Mbali na La-Nina pia kuongeze kidogo kwa joto la bahari Mashariki mwa bahari ya Hindi ukilinganisha na Magharibi mwa bahari ya Hindi kunasababisha kuwepo kwa upepo hafifu wenye unyevunyevu unaovuma kuelekea maeneo mengi ya nchi, hivyo kusababisha msimu wa vuli kuwa na mvua za wastani au maeneo mengine kupata mvua chini ya wastani,” amesema.
Amesema, kwenye maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na ya Pwani ya Kaskazini hali itakuwa mbaya zaidi kwani katika maeneo hayo mvua za msimu wa vuli zitakuwa chini ya wastani kuelekea wastani.
“Maeneo mengi ya nchi zaidi yale ukanda wa Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na Pwani ya Kaskazini yakihusisha maeneo ya Kaskazini ya mkoa wa Morogoro na Kaskazini ya mkoa wa Kigoma kwa ujumla yatapata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
“Maeneo ya Ukanda wa Ziwa peke yake yanatazamiwa kuwa na mvua za wastani,” amesema Dk Kantamla.