Bagamoyo. Moja ya sababu ya kuibuka kwa migongano baina ya binadamu na wanyamapori ni kufanyika kwa shughuli za kibindamu kwenye shoroba.
Shoroba ni njia za asili ambazo hutumiwa na wanyamapori kama tembo katika harakati za kutoka eneo moja kwenda jingine, nje ya maeneo ya hifadhi, kutafuta mahitaji yao kama chakula na maji.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Septemba 5, 2024 na Ofisa Mhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Isaac Chamba wakati akitoa mada kwenye mafunzo juu ya uandishi wa habari za migongano baina ya binadamu na wanyamapori Tanzania.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).
“Mfano, jengo la Halmashauri ya Mvomero mkoani Morogoro,” amesema.
Chamba amesema sababu nyingine ya migongano hiyo ni kutokuwapo kwa matumizi bora ya ardhi, uvamizi wa mifugo eneo la hifadhi, mabadiliko ya tabianchi na jamii kuamini imani potofu.
Amesema asilimia 80 ya matukio hayo yanasababishwa na tembo.
“Changamoto hizi zinatokea nje ya hifadhi, hivyo ni muhimu jamii ihamasishwe kutumia mbinu mbalimbali kuepuka changamoto.
“Shoroba ni muhimu kwa wanyamapori, ukiziba mnyama hajui, yeye atapita tu hata ikipita miaka 40,” amesema.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori unaotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania kwa miaka mitano, unaofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia shirika la GIZ.
“Na mradi umelenga katika ukanda wa Ruvuma, kwa maana ya mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Tunduru, Wilaya ya Namtumbo na Wilaya ya Liwale.
Kazi kubwa ambazo tunazifanya kwenye mradi huu ya kwanza ni kufundisha waandishi wa habari ambao mafunzo ya kwanza tulishafanya mwezi wa pili, lakini pia tuna mkutano na wahariri wa vyombo vya habari kutoka wanachama au waandishi wanaotekeleza mradi huu.
Pia, tunakuwa na breakfast debate midahalo mbalimbali ipatayo Minne, tumeshafanya mmoja na tunategemea wiki ijayo Septemba 11 tutafanya mdahalo mwingine, pia tunapeleka waandishi hawa ambao wamepata mafunzo maeneo husika,” Chikomo.