VIONGOZI HALMASHAURI YA MPWAPWA WAASWA KUFANYA KAZI KWA KUSHIRIKIANA

 

Katibu Msaidizi Kanda ya Kati Dodoma kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,Bi.Jasmin Awadhi, akitoa mafunzo ya uwajibikaji wa pamoja kwa waheshimiwa madiwani na wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya wilaya ya Mpwawa, mafunzo yalifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mpwapwa

Washiriki wa mafunzo ya uwajibikaji ambao ni waheshimiwa madiwani pamoja na wakuu wa Idara na vitengo wa Halmashauri ya wilaya ya Mpwawa wakifuatilia kwa makini mafunzo hayo yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpwapwa Mhe. George Rume akifungua mafunzo yaliyohusu uwajibikaji wa pamoja kwa waheshimiwa madiwani na wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya wilaya ya Mpwawa, mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati yalifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mpwapwa

….

Viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambao ni madiwani pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo wameaswa kuzingatia dhana nzima ya uwajibikaji wa pamoja wakati wanatekeleza majukumu yao ya kila siku ili kuweza kuwaletea wananchi maendeleo kuipatia serikali mafanikio.

Wito huo umetolewa na Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili Kanda ya Kati – Dodoma Bi. Jasmin Awadh wakati akitoa mafunzo hayo kwa viongozi hao yaliyofanyika katika Halmashauri hiyo tarehe 05 Septemba, 2024

Aidha Bi. Jasmin alieleza kuwa suala la uwajibikaji wa pamoja kwa Viongozi lisipozingatiwa litasababisha ucheleweshwaji wa huduma za kijamii kwa wananchi kama vile hospitali, shule,  barabara n.k na wananchi watapoteza imani yao kwa serikali.

”Kunapokua na mkinzano baina ya viongozi juu ya namna ya utekelezaji wa huduma mbalimbali  za kijamii huyu anasema tufanye vile yule anasema tufanye  vile lazima huduma hizo zikwame ama kutokufanyika kabisa”

Bi.Jasmin aliwahimiza viongozi hao kushirikiana katika kupanga vipaumbele vya Taasisi ili kuhakikisha kwamba malengo yaliyopangwa na halmashauri yanatekelezwa ipasavyo ikiwemo kuwafikishia wananchi huduma wanazohitaji.

“Nyinyi kama Viongozi mnapaswa kuwashirikisha watumishi walio chini yenu juu ya mikakati mliyonayo ili muweze kushirikiana kuitekeleza mnapaswa nyote muwe na uelekeo mmoja kila mtumishi aelewe jukumu lake katika kufanikisha malengo ya Taasisi”

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa Mhe. George Rume alisema kuwa mafunzo hayo kwa viongozi hao ni muhimu sana kwani yatawasaidia kuleta mabadiliko katika halmashauri yao kwani suala la maadili ni la muhimu sana hasa ushirikiano na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yetu.

Kwa mujibu wa Mhe Rume alieleza kuwa kiongozi yeyote ni lazima ajue dira ya Taasisi yake kwamba nini anatakiwa kufanya  ili aweze kuwaongoza walio chini yake kuitekeleza na kuleta maendeleo kwa wananchi na serikali kwa ujumla. 

”Tukianza kukinzana viongozi kwa viongozi hatufiki popote na tutazorotesha juhudi za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo’’ alisema.

Mafunzo hayo ni mkakati na kipaumbele cha Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhakikisha kwamba Viongozi wote wanashirikiana katika Taasisi zao wanafanya kazi kwa pamoja kwa kuzingatia viwango vya juu vya maadili na kuleta matunda kwa wananchi 

Related Posts