Wananchi wahamasishwa kupata elimu ya fedha kujikwamua

Dar es Salaam. Elimu ya fedha kwa wananchi imetajwa kuwa jambo la muhimu kwa kuwa itawawezesha kutumia kwa malengo kiasi wanachokipata katika kazi zao.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 5, 2024 jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha Dk Charles Mwamwanja wakati akizindua Mfuko wa Inuka.

Amesema usimamizi mzuri wa fedha ndiyo unaohitajika kwa ajili ya kupanga mipango mizuri ya namna ya kutumia kiasi kidogo unachokipata baada ya kufanya kazi mbalimbali.

“Ukipata pesa unaweza kuzitumia mara moja au ukaamua kuziwekeza na kimsingi uwekezaji ni mzuri sana kwa sababu unajali maisha yajayo.

“Lakini jambo zuri kuhusu Inuka Fund ni kwamba kiasi unachoweza kuanza kuwekeza ni Sh10,000 tu ambacho ni kiwango kikubwa kama Watanzania wengi wanaweza kumudu,” amesema/

Ameongeza kwamba mbali na kiasi hicho cha awali cha uwekezaji, mtu anaweza kuendelea kuwekeza hata ukiwa na Sh1,000 na wanatumia majukwaa ya simu katika kurahisisha mchakato mzima ambao unapendekezwa.

Ameutaka Mfuko wa Inuka na wadau wao kuja na mikakati ya elimu ya fedha pamoja na kuhakikisha Watanzania wengi wanafikiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Orbit Securities, Godfrey Malauri amewataka Watanzania kutumia Inuka Fund kila wanapotaka kuwekeza fedha zao.

“Jambo la kipekee kuhusu Inuka Fund ni kwamba mwekezaji yuko huru kujiunga na kuondoka kwenye mpango huo wakati wowote, unatoa urahisi kwa watu,” anasema.

Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Alfred Mkombo amebainisha kuwa Mfuko wa Inuka ni miongoni mwa taasisi zinazodhibitiwa na CMSA.

“Niwasihi Watanzania kuwa waangalifu wanapochagua wapi wanataka kuwekeza fedha zao na kila wakati watafute ile ambayo imedhibitiwa nasi.

“Pia, ukiwa na Mfuko wa Inuka unapata mapato ya kutosha ndiyo maana tunasisitiza Watanzania wenzetu kuwekeza kwenye chombo hiki kwa manufaa yao,” amesema.

Related Posts