Arusha: Wananchi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajia kunufaika na fursa nyingi zaidi za kibiashara kupitia jukwaa la pamoja la biashara mtandaoni linalotarajiwa kuanzishwa na EAC.
Hatua hiyo inafuatia ombi la Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), Adrian Njau, kwa uongozi wa EAC wakati wa mkutano wa wadau wa biashara mtandaoni kutoka nchi za Afrika Mashariki na mashirika ya kimataifa.
Mkutano huo, ulioratibiwa na EABC kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Ujerumani Kanda ya Afrika Mashariki (GIZ-EAC), umelenga kujadili utekelezaji wa mikakati ya kikanda ya biashara mtandaoni na athari zake kwa nchi za EAC.
Njau amesema kuanzishwa kwa jukwaa hilo la pamoja la biashara mtandaoni kutaimarisha uchumi wa wanachama wa EAC na kuchochea maendeleo ya kikanda kwa ujumla.
Ofisa Mkuu wa Biashara wa EAC, Angelique Umulisa, ameeleza kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya kidijitali, biashara mtandaoni inatoa fursa kubwa kwa ustawi wa uchumi wa EAC.
Ameahidi kuanza kujadili utekelezaji wa jukwaa hilo kwa haraka.
Ameongeza kuwa idadi kubwa ya vijana, ambao ni zaidi ya asilimia 60 ya watu katika EAC, wanapaswa kutumia fursa za kielektroniki ili kufaidika zaidi kwenye soko la biashara mtandaoni.
Hata hivyo, changamoto kubwa zinazoikabili biashara mtandaoni imeelezwa ni pamoja na gharama za uendeshaji, ukosefu wa ujuzi wa kusimamia na kuendesha biashara hizo, ufinyu wa miundombinu na upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, EAC imeanzisha mkakati wa kikanda wa biashara wa kielektroniki wa miaka 10, unaolenga kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa mtandao, usalama wa biashara mtandaoni, ulinzi wa data, na mwingiliano wa mifumo ya malipo.
Njau, akifungua mkutano huo, amesisitiza umuhimu wa kuanzisha jukwaa hilo ili kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuwezesha biashara kuvuka mipaka kwa urahisi zaidi.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kuanza na utafiti kwenye sekta binafsi ili kujifunza kutoka kwa uzoefu wa biashara za mtandaoni, mafanikio yao, na changamoto walizokumbana nazo. Hili litasaidia kuandaa mikakati bora ya ukuaji wa biashara hiyo.
Njau amesema ni lazima kuwepo mipango madhubuti kama vile biashara ya kielektroniki mipakani, malipo ya kidijitali, ujumuishaji wa kifedha na mazoea endelevu ili kuunda mfumo wa kidijitali unaofanya kazi vizuri na unaojumuisha watu wengi.
“Ili kukabiliana na changamoto hizi, EAC imepitisha Mkakati wa Kikanda wa Biashara wa Kielektroniki wa miaka 10 na zinazolenga kuimarisha ulinzi wa watumiaji mitandao, usalama wa mtandao kibiashara, ulinzi wa data na mwingiliano wa mfumo wa malipo,” amesema.
Odo Yaramba, mshauri wa biashara ya kidigitali kutoka GIZ, ameeleza umuhimu wa biashara mtandaoni kwa ushirikiano kati ya wadau wa huduma za biashara za mtandaoni, huku akisisitiza kuwepo mikakati ya pamoja na majukwaa ya kujengeana uwezo.
Amezihimiza nchi za EAC kuendelea kuhamasishana na kujenga majukwaa mengi zaidi ili kutambua changamoto mapema na kuweka mbinu za kuzitatua.
“Mnapaswa kuwa na majukwaa kama haya zaidi ili kuzitambua changamoto na kupanga mbinu mapema ya kukabiliana nazo,” amesema.