KANISA LA KIASKOFU ANGLILANA JIMBO JIPYA LA TANZANIA WAOMBA USHIRIKIANO WA SERIKALI

.Askofu wake wa kwanza nchini kusimikwa Septemba 15, watoa neno kuhusu sadaka

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

KANISA la Kiaskofu la Anglikana jimbo jipya la Tanzania, limeiomba serikali kushirikiana nayo kuleta maendeleo katika sekta ya elimu, maji, afya, michezo na miundombinu, hasa sehemu za vijijini.

Mbali ya kuomba ushirikiano na Serikali ,Septemba 15 Mwaka huu kanisa hilo litamsimika askofu wake mkuu wa kwanza hapa nchini, Elibariki Kutta, katika misa takatifu itakayofanyika Mlale, Kongwa mkoani Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 6,2014 Jijini Dar es Salaam Askofu Kutta amefafanua kwa kina kuhusu Kanisa hilo limeanzishwa kwa madhumuni ya kuirejesha Anglikana katika historia na utamaduni wake wa kuhudumia jamii pamoja na kubadilisha maisha ya watu na kupinga mambo maovu.

Akieleza zaidi Askofu Kutta amesema mwaka 1885 hadi Tanzania ilipopata uhuru wake mwaka 1961, kanisa hilo lilikuwa likiendesha miradi ya shule, hospitali na huduma nyingine muhimu kwa manufaa ya jamii lakini kwa sasa kinyume chake.

Ameongeza kwamba waumini hawana uhuru wa kuhoji chochote badala yake miradi imebaki kunufaisha zaidi viongozi na kusisitiza hata sadaka ambazo waumini wanatoa zimekuwa haziwanufaishi wao na badala yake zinanufaisha baadhi ya viongozi wa Kanisa.

“Kuhusu sadaka sisi Kanisa la Kiaskofu la Kianglikana jimbo jipya la Tanzania, tunataka sadaka zote ambazo zitakazokuwa zinatolewa na waumini zibaki kwa maendeleo yao katika maeneo husika hususan vijijini.

“Tunataka sadaka za sehemu moja zinufaishe katika parokia hiyo hiyo badala ya kupelekwa kwingine.Tunataka waumini wanufaike na sadaka wanazotoa badala ya kuacha Askofu ndio anayepanga matumizi ya hizo sadaka,” amefafanua

Kuhusu kuanzishwa jimbo jipya la kanisa hilo nchini Tanzania Askofu Kutta ameeleza kwamba wao bado ni waumini wa Waanglikana na hawajasambaratika, bali wanachofanya ni kuanzisha kanisa huru litakalokuwa linajali zaidi mahitaji ya watu lengo letu sadaka zibadili maisha yao.

Ameongeza pia kanisa la Kiaskofu la Kianglikana linataka waumini wenye uhuru wa kutoa mawazo, ikiwamo kupinga uovu ndani ya kanisa akitaja baadhi ni vitendo vya ushoga, usagaji na utoaji mimba ambavyo ni kinyume na maandiko matakatifu.

Akizumgumzia kuhusu kusimikwa kwa Askofu wake Mkuu Jimbo la Tanzania amesema tukio hilo litashuhudiwa pia Askofu Mkuu wa Maaskofu Wakuu wa kanisa hilo duniani, Mark Haverland kutoka nchini Marekani ambaye ndio ataendesha Misa.

Kuhusu kuomba serikali kushirikiana na Kanisa hilo Askofu Kutta amesema anaamini ushirikiano baina yao utasaidia Kanisa hilo kuchagiza maendeleo kwa maeneo ya vijijini ambako maendeleo yapo nyuma zaidi ikilinganishwa na mijini.

Amesisitiza kuwa pamoja na kuiunga mkono Serikali lakini wanatamani kushirikiana na Rais Dk Samia Suluhu Hassaan ambaye amedhamiria kumtua ndoo mama kichwani na Kanisa hilo liko tayari kusaidia kuondoa changamoto ya uhaba wa maji safi na salama.

“Tunaiunga mkono sera ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani, hivyo tunaiomba serikali ishirikiane nasi katika azma ya mheshimiwa Rais kwa wananchi wa vijijini kupata maji tiririka, safi na salama.”

Kwa upande wake Mwakilishi wa Askofu Mkuu Haverland, Zah Freeman, amesema wanataka kanisa libaki kuwa huru kama ilivyokuwa katika miaka ya 1885 hadi uhuru wakati linaanzishwa na Wamisionari tofauti na lilivyo hivi sasa.


Related Posts