Mahakama yabariki kifungo cha maisha aliyelawiti mtoto wa miaka mitatu

Arusha. Mahakama Kuu imebariki adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa mkazi wa Tandahimba, Baraka Katembe, aliyohukumiwa kwa kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka mitatu.

Mahakama imefikia uamuzi huo katika hukumu iliyotolewa na Jaji Martha Mpaze, Septemba 3, 2024, baada ya kutupilia mbali rufaa ya Baraka ya kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Tandahimba.

Baada ya kupitia mwenendo na kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Mpaze amesema Mahakama inatupilia mbali akisema upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka yoyote.

Mahakama ya Wilaya ya Tandahimba ilimtia hatiani Baraka katika kesi ya msingi ya jinai namba 73/2023, baada ya kushawishika na ushahidi wa mashahidi sita wa upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo, ilidaiwa Oktoba 15, 2023 jioni, katika Kijiji cha Mdumbwe, Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, Baraka alishtakiwa kwa kosa la kumwingilia kinyume na maumbile mtoto huyo mwenye umri wa miaka mitatu.

Baraka alidaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 154 (1) (a) na (2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (PC).

Ilidaiwa na shahidi wa tatu na nne kuwa siku ya tukio, wakiwa wanacheza nje ya nyumba ya Baraka, walisikia sauti ya mwathirika wa tukio hilo akilia ndani ya nyumba na walipoenda ndani walimkuta akiwa uchi amelala kwenye kitanda cha Baraka ambaye kwa wakati alikuwa alikuwa nusu uchi.

Baba wa mwathirika huyo, alidai kuwa akiwa shambani alipata taarifa za tukio hilo na akiwa njiani alikutana na Baraka, akamkamata na kumrudisha nyumbani kwake ambako alikutana na watu wengi walioamua kumpeleka polisi.

Daktari aliyemfanyia mtoto huyo uchunguzi, alidai baada ya uchunguzi huo alibaini michubuko katika sehemu ya haja kubwa ya mtoto huyo na mbegu za kiume.

Hata hivyo, ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo haukurekodiwa kwa sababu hakuwa na uwezo wa kujibu swali lolote lililoulizwa.

Katika utetezi wake, Baraka alidai kesi hiyo ni ya uzushi kwa kuwa alikuwa na mgogoro wa shamba na baba wa mtoto huyo na kuwa baba huyo alimwambia ‘utaona’ na siku iliyofuata alimkamata akimtuhumu amemlawiti mtoto wake.

Licha ya utetezi huo, mahakama ilibaini upande wa mashtaka umethibitisha kesi bila kuacha shaka na kumhukumu Baraka kifungo cha maisha jela.

Katika rufaa hiyo Baraka ambaye hakuwa na wakili, alikuwa na hoja tisa za rufaa ikiwemo upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi yake pasipo kuacha shaka, hakimu hakuzingatia masharti ya lazima ya kifungu cha 127(2) cha Sheria ya Ushahidi na kwamba hajawahi kukiri kutenda kosa hilo.

Upande wa Jamhuri uliowakilishwa na Wakili wa Serikali Edson Mwapili ulieleza kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha pasipo kuacha shaka kesi hiyo.

Kuhusu kukiri kosa hilo, wakili huyo alisema kushindwa kukiri hakumaanishi kuwa hakutenda kosa, alisema kwa ushahidi uliopo umethibitisha alitenda kosa hilo.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Mpaze amesema alipochunguza mwenendo wa kesi hiyo aligundua ushahidi ambao ulipaswa kutolewa kwa mujibu wa kifungu cha 127 (2) ni wa shahidi wa pili (mwathirika), tatu (mwenye umri wa miaka minane) na nne (mwenye umri wa miaka sita).

Ameeleza kuwa mahakama ilitoa sababu za kutochukua ushahidi wa mwathirika na hivyo hawezi kuhitimisha kuwa kifungu cha 127(2) hakikuzingatiwa.

Kuhusu shahidi wa tatu na nne, kabla ya ushuhuda wao kuchukuliwa, utaratibu uliohitajika ulifuatwa na wote wawili waliahidi kutozungumza chochote isipokuwa ukweli.

Kuhusu kesi kutothibitishwa, Jaji aliungana na Wakili Mwapili kuwa jukumu la msingi la upande wa mashtaka lilikuwa kuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.

Alisema shahidi wa sita aliyemchunguza mwathiriwa, aliweza kuthibitisha kwamba mwathirika alikuwa chini ya umri wa miaka 18,” amesema Jaji.

Jaji Mpaze amesema Baraka hakubainisha ni ushahidi gani hasa haukuwa na uthibitisho, kwani ni muhimu kutambua ushahidi uliotolewa katika kesi hii ulikuwa wa kutosha,” ameongeza jaji.

Kuhusu hoja ya kuamua suala la nani alitenda kosa hilo, Jaji amesema amezingatia utetezi wa Baraka, japo hajakubaliana nao.

“Yote yaliyosemwa naona rufaa haina mashiko, kwa hiyo ninaikataa na nimezingatia utetezi wa mrufani ingawa sikubaliani nao, naona upande wa utetezi haujatikisa kwa namna yoyote ile kesi ya upande wa mashtaka,” amesema.

Related Posts