Songea. Mahakama Kuu Kanda ya Songea, imelikataa ombi la mfugaji mkazi wa Tunduru, Leleshi Ratu la kutaka Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tunduru, azuiwe kuendelea na operesheni ya kukamata mifugo na kutoza faini.
Katika uamuzi alioutoa jana Septemba 5, 2024 kuhusu maombi namba 20169 ya 2024 dhidi ya DC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Emmanuel Kawishe amesema kutoa amri hiyo itakuwa ni sawa na ‘kuweka mkokoteni mbele ya farasi’ msemo unaomaanisha kufanya jambo kinyume cha utaratibu au kuanza na jambo lisilo sahihi kabla ya kushughulikia hatua muhimu.
Kwa mujibu wa kiapo, Ratu alieleza yeye ni mfugaji anayeishi katika vijiji vya Mkowela na Liwangula na kwamba, katika kila kijiji anamiliki ng’ombe ambao wanapata malisho katika maeneo anayoyamiliki.
Alieleza Agosti 7, 2024 saa 10.00 alasiri, askari polisi akiwa amefuatana na watumishi wa ofisi ya DC Tunduru, walifika eneo analolitumia kuhifadhi mifugo na kuichukua, kisha kuipeleka uwanja wa Shule ya Msingi Ngalije.
Mifugo ikiwa katika uwanja huo, alitakiwa kulipa faini ya Sh23, 500 kwa kila ng’ombe na kwa ng’ombe 144, alitakiwa kulipa faini ya Sh3.38 milioni, ambayo alisema haina uhalali kisheria.
Muombaji huyo, alisema operesheni ya kukamata ng’ombe kwa nguvu imekuwa ikitokea kila mwaka kuanzia Agosti hadi Oktoba na kwamba, imekuwa ikiwaathiri wafugaji akiwamo yeye anayemiliki eneo la malisho.
Aliiomba mahakama itoe kibali kwake cha kufungua maombi ya kuitaka itoe amri kumzuia DC Tunduru kukamata ng’ombe na kutoza faini. Ombi ambalo lilipingwa na DC Tunduru na AG kupitia kiapo.
Wakati maombi hayo yalipoitwa kusikilizwa kwa mara ya kwanza Agosti 29, 2024, mfugaji huyo aliwakilishwa na Wakili Benedict Pius, wakati wajibu maombi waliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Egidy Mkolwe na Ibrahim Kabelwa.
Siku hiyo wakili Pius aliwasilisha maombi, moja likiwa kwamba Mahakama iwaruhusu kuwasilisha maelezo ya nyongeza katika kiapo cha Ratu, akieleza kuna taarifa muhimu zinapaswa kuingia ili kuyapa nguvu maombi yake.
Ombi la pili alilikuwa la kupatiwa kibali cha kumshtaki DC ambalo halijasikilizwa lakini operesheni ya kukamata mifugo na kutoza faini ilikuwa linaendelea, hivyo aliiomba mahakama itoe amri kuzuia operesheni hadi ombi lao litakaposikilize.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Mkolwe alisema ombi la msingi lililopo mahakamani ni kupata kibali cha kumshitaki DC Tunduru, hivyo kuomba amri ya kusimamisha operesheni inayofanywa na DC Tunduru siyo sahihi kisheria.
Alieleza ombi la wakili huyo la kuomba amri ya kusitisha operesheni hiyo limeletwa kabla ya muda, kwa kuwa tayari amewasilisha ombi kwa mahakama ili itoe amri itakayowaruhusu kuongeza taarifa kwenye kiapo chao.
“Kabla hata ombi hilo mbele ya mahakama halijakubaliwa ili kuona nini kimeongezwa katika kiapo hicho, amekuja na ombi linguine, jambo ambalo si mbinu sahihi kwa kuwa ombi hilo limezuiwa na ombi lake la kuongeza taarifa,” alidai.
Jaji Kawishe katika uamuzi wake alisema baada ya kusikiliza mawasilisho ya pande zote mbili, anaona hoja ya msingi katika maombi hayo ni kama amri ya kuzuia operesheni ya DC Tunduru itolewe katika maombi hayo mapya.
“Ni muhimu kufahamu kuwa maombi ya msingi ni kwa ajili ya kupatiwa kibali cha kufungua maombi ili kupata amri ya kumzuia mjibu maombi wa kwanza (DC Tunduru) kutaifisha mifugo ya wafugaji na kuitoza faini,” amesema.
“Lakini kabla maombi hayo hayajasikilizwa kwa ukamilifu na kutolewa uamuzi, wakili wa mleta maombi anaomba amri ya kumzuia mjibu maombi wa kwanza kuendelea kukamata mifugo ya wafugaji na kutoza faini, ambalo ndilo ombi kuu,” amesema.
Jaji amesema, “kwa maoni yangu, maombi ya msingi katika shauri hilo ambayo kama yatasikilizwa na kutolewa uamuzi na Mahakama ni kutolewa kwa kibali ili mleta maombi afungue shauri la kutaka amri ya kumzuia DC kukamata mifugo.
“Kama Mahakama itakubali kutoa amri ya kumzuia DC Tunduru kukamata mifugo, itakuwa ni sawa na kuweka mkokoteni mbele ya farasi. Mara tu baada ya kutolewa kwa amri hiyo, kutakuwa hakuna haja ya kusikiliza ombi la msingi.
“Kutakuwa hakuna haja ya kusikiliza ombi la mleta maombi la kuruhusiwa kuongeza taarifa kwenye kiapo chake. Kutoa amri ya kumzuia DC kukamata mifugo na kutoza faini itakuwa ni sawa na kitendo cha kutoa mimba.”
Amesema kufanya hivyo itakuwa ni kufanya jambo lililo mbele yake liwe limepitwa na wakati, hivyo anayatupa maombi na badala yake, anaamuru ombi la kupatiwa kibali lisikilizwe kwanza.