Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema msingi wa ushindi wa chama chochote cha siasa katika uchaguzi ni kuhakikisha wananchi wanajitokeza kushiriki michakato yote ya kuelekea uchaguzi.
Michakato hiyo inahusisha kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpigakura na kushiriki kupiga kura.
CCM inakuja na kauli hiyo ikiwa imesalia miezi mitatu kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu, ukilenga kuwapata wawakilishi wa wananchi ngazi ya vijiji, mitaa na vitongoji.
Akizungumzia hilo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla anasema ni muhimu wanachama wa chama hicho na vyama vingine wajitokeze kujiandikisha katika daftari la wakazi litakaloanza Oktoba 11, mwaka huu.
Akiwa katika ziara ya kuimarisha chama hicho mkoani Arusha, Makalla anasema kuna umuhimu wa uchaguzi huo ndiyo maana wananchi wanapaswa kuhakikisha wanashiriki ama kujitokeza wachaguliwe au wajitokeze wachague wawakilishi wao.
Anasisitiza kwa kuwataka wananchi wasifikirie kuupuuza uchaguzi huo kwa kile alichoeleza kuwa ni msingi wa mabadiliko katika maeneo ya mitaa, vijiji na vitongoji.
“Ili tushinde tunahitaji kujiandikisha, ushindi wowote ni idadi ya kura, tujiandikishe katika daftari la wakazi litakaloanza Oktoba 11 hadi 20, hata kama una kadi ya kupigia kura hicho ni kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
“Oktoba 10 uwe na kadi au usiwe nayo lazima ukajiandikishe ili kuwa na uhakika wa kupiga, usikae na kadi ukafikiri utapiga kura hutasomeka kwenye daftari la wakazi, hilo ndiyo kubwa na muhimu sana,” anasema Makalla.
Kwa kuwa michakato ya kuelekea uchaguzi inahusisha siku kadhaa, amewataka wanachama wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanatenga siku 10 kwa ajili ya kujiandikisha na hatimaye wapige kura.
“Kuna siku ya mnada, kliniki au kuna siku ya mtoto mambo ya shule lakini tenga siku moja twende ukapate haki yako ya kukipa ushindi CCM,” anasema Makalla.
Akizungumzia chama chake, Makalla anasema makada wa Mkoa wa Arusha na Manyara, wanapaswa kuthamini na kuuchukulia kwa uzito mkubwa mchakato na kujitokeza kwa wingi kwani ndiyo mtaji wa ushindi.
“Lengo la chama chochote cha siasa ni kukamata dola kwa hiyo ndugu zangu kwa mfumo wa uchaguzi wa Tanzania ili ushike dola, kuna chaguzi mbili uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kwa hiyo uchaguzi huu una umuhimu wa kushinda.
“Tusidharau, tusibweteke tuweke malengo serikali za mitaa tushinde kwa kishindo, upo umuhimu na sababu za sisi kwenda kuwashawishi wenzetu wanachama, marafiki zetu wapenda maendeleo, watu wanaokipenda Chama cha Mapinduzi watuazime imani hiyo ya kukichagua,” anasema Makalla.
Makalla anasema umuhimu wa uchaguzi ndiko chimbuko la utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoanzia katika ngazi ya mitaa, vijiji na vitongoji kwa viongozi wa maeneo hayo kupanga maendeleo na kuyafikisha ngazi ya juu.
Anasema chama hicho kimedhamiria kuibuka kidedea katika uchaguzi huo.
Anasema chama hicho kitawateua wagombea wenye sifa watakaopeperusha vyema bendera ya CCM.
“Niseme CCM itahakikisha inateua wagombea safi wasio na makandokando mwenyekiti wa wilaya kamati yako ya siasa, halmashauri yako kuu ya wilaya dhamana hii tunawaachia ninyi mtateua kwa niaba ya CCM.
“Hakikisheni mnateua watu wanaokubalika wasiokuwa na kashfa, watu ambao matatizo ya kijiji wao ni sehemu yao, wawe watu wa kutatua kero hizo,” anasema.
Makalla anasema kuna kilio wakati mwingine kero na ugumu wa CCM unatokea kwa sababu kuna baadhi ya wenyeviti waliopewa dhamana hawasomi taarifa za mapato na matumizi.
“Bado nina harufu ya ukuu wa mkoa wa Mwanza, wakati ule kila ukienda unauliza mna kero hapa? tunaona kazi zinakwenda na fedha zinaletwa unaambiwa shida yetu ni mapato na matumizi, yaani mnataka kunyimwa kura kwa sababu ya mtu mmoja.
“Asiyesoma taarifa ya mapato na matumizi, katika uchaguzi ujao hawana nafasi ndani ya CCM, jitahidini kuteua wagombea wanaoishi vizuri na watu siyo sehemu ya makandokando,” anasema.
Makalla ambaye yupo katika ziara ya siku sita katika mikoa ya Arusha na Manyara pamoja na mambo mengine, ikiwemo kusikiliza kero za wananchi wa maeneo anayotembelea anatumia muda huo kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uchaguzi wa serikali mitaa, vitongoji na vijiji.
Kila anapopita iwe kuzungumza na wananchi au kusalimiana na wana-CCM, Makalla amekuwa mstari wa mbele kuzungumzia suala la uchaguzi huo, akiwataka wanachama wa chama hicho kuwahamasisha Watanzania kujitokeza kushiriki uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa Makalla, kwa namna Serikali ilivyotekeleza ilani ya chama hicho tawala, CCM haihitaji mbeleko katika chaguzi zijazo ukiwemo wa serikali za mitaa na vijiji na vitongoji kwa sababu miradi mingi ya maendeleo inayowagusa wananchi imetekelezwa.
Suala la kuhamasisha watu kujitokeza kushiriki katika uandikishaji wa daftari la wakazi lilitiliwa mkazo na viongozi wa CCM Mkoa wa Arusha wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, mkoani humo Loi Thomas Ole Sabaya.
Ole Sabaya aliwataka Wana-CCM kujitokeza kushiriki mchakato huo, akisema chama hicho kimejipanga vyema kuhakikisha kinaibuka kidedea kwenye uchaguzi huo kwa kunyakua mitaa, vitongoji na vijiji vingi.
Uchaguzi wa serikali za mitaa nchini ni mchakato wa kidemokrasia unaoruhusu wananchi kuchagua viongozi wa ngazi za chini katika jamii. Uchaguzi huu unahusisha kuchagua viongozi wa vijiji, vitongoji, na miji midogo.
Serikali za mitaa ni mihimili muhimu ya usimamizi wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii. Huu ni uchaguzi unaolenga kuleta uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi yanayohusu maisha yao ya kila siku.
Uchaguzi wa serikali za mitaa unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287 ya mwaka 1982.
Aidha, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288, nayo inaweka misingi ya kisheria kwa maeneo ya miji. Sheria hizi zinafafanua taratibu za uchaguzi, majukumu ya viongozi wanaochaguliwa, na haki za wananchi katika mchakato huo.
Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) kinaeleza kuwa, “Uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa utafanyika kila baada ya miaka mitano kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa na Tume ya Uchaguzi.”
Hii inatoa mwelekeo wa kipindi cha uchaguzi na kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa utaratibu wa kidemokrasia.
Pia, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, inatoa maelekezo kuhusu jinsi ya kuendesha uchaguzi huu ili kuhakikisha unakuwa huru na wa haki.
Kifungu cha 6(2) cha sheria hii kinasema, “Wapiga kura wote watakuwa na haki sawa ya kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi.”
Uchaguzi wa serikali za mitaa hufanyika kila baada ya miaka mitano. Kwa kawaida, uchaguzi huu huandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ina jukumu la kuandaa ratiba ya uchaguzi, kuainisha wapiga kura waliojiandikisha na kusimamia shughuli nzima ya uchaguzi.
Sheria inalazimisha kutangazwa kwa uchaguzi mapema ili kuruhusu wananchi na wagombea kujipanga ipasavyo.