MBOWE ATAKA FIDIA YA BILIONI 5 KWA MSIGWA – MWANAHARAKATI MZALENDO

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amemtaka Mchungaji Peter Msigwa, ambaye kwa sasa amehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kulipa fidia ya shilingi bilioni tano (5,000,000,000/=) kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutoa taarifa za uongo dhidi yake. Kulingana na taarifa ya mawakili wa Mbowe kutoka Matwiga Law Chambers, Msigwa anatuhumiwa kwa kueneza maneno yanayodaiwa kuchafua taswira ya Mbowe kisiasa, kidini, kirafiki, na kifamilia.

Tuhuma hizo zinahusiana na matamshi ya Msigwa yaliyotolewa kupitia jukwaa la Clubhouse, katika kipindi cha maswali na majibu kilichoitwa Taifa Kwanza Hajji305. Katika mazungumzo hayo, Msigwa alinukuliwa akidai kuwa Mbowe anamiliki Mbowe Foundation, ambayo inadaiwa kuwa inafanya kazi ya kuendesha CHADEMA. Pia alidai kuwa Mbowe ana helkopta na anatembea na msafara wa magari zaidi ya kumi, jambo ambalo linadaiwa kuwa na athari mbaya kwa taswira ya kiongozi huyo.

Mbali na fidia hiyo, mawakili wa Mbowe wamemtaka Msigwa kuomba radhi hadharani ndani ya siku tano tangu tarehe 4 Septemba 2024, kupitia magazeti mawili, moja la kitaifa na jingine la kikanda. Pia Msigwa anatakiwa kukiri kwamba hatotumia nafasi yake vibaya tena katika jamii.

Katika barua hiyo, mawakili wa Mbowe wameandika wazi kuwa Msigwa anatakiwa kulipa kiasi cha shilingi bilioni tano kama adhabu ya kumchafua Mbowe na kuharibu taswira yake mbele ya jamii. Mawakili wanaomwakilisha Mbowe ni John Mallya, Jonathan Mndeme, Hekima Mwasipu, Simon Mrutu, na Dickson Matata kutoka Matwiga Law Chambers.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts