Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa Telegram, Pavel Durov, amekana vikali madai ya kutokudhibiti matumizi mabaya ya programu yake, baada ya kukamatwa mnamo Agosti 25, 2024. Durov alikamatwa kwenye uwanja wa ndege kaskazini mwa Paris na baadaye kushtakiwa kwa madai ya kushiriki kuruhusu miamala haramu, ulanguzi wa dawa za kulevya, ulaghai, na kusambaza picha za unyanyasaji wa watoto kupitia jukwaa la Telegram.
Katika taarifa yake, Durov alisema madai hayo ni “upotoshaji” wa hali halisi na akaongeza kuwa si sahihi kumshikilia yeye binafsi kuwajibika kwa uhalifu uliofanywa na watumiaji wachache kwenye jukwaa hilo. Alieleza kuwa, “kutumia sheria za enzi za kabla ya simu mahiri dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji kwa uhalifu wa watumiaji ni mbinu potofu.” Durov alisisitiza kuwa, ikiwa nchi inahitaji kuchukua hatua, inapaswa kuelekeza juhudi hizo kwa kampuni yenyewe, si kwa watu binafsi.
Durov alikanusha vikali madai kwamba Telegram ni “paradiso ya machafuko,” akisema kuwa kampuni hiyo inaondoa mamilioni ya machapisho na chaneli zenye madhara kila siku. Hata hivyo, alikubali kwamba ongezeko kubwa la watumiaji hadi milioni 950 limeleta changamoto za kiusalama, na akasisitiza kuwa kampuni inafanya kazi kuboresha mifumo yake ya kudhibiti maudhui.
Matamshi haya yanakuja baada ya ripoti kuonyesha kuwa Telegram imekataa kujiunga na programu za kimataifa za kugundua na kuondoa nyenzo za unyanyasaji wa watoto mtandaoni. Hata hivyo, Durov aliweka wazi kuwa Telegram ina mwakilishi rasmi katika Umoja wa Ulaya na imekuwa ikishirikiana na mamlaka inapohitajika.
#KonceptTvUpdates