MKURUGENZI WA TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI AAGIZA WAKANDARASI KUTOKA HARAKA KUMALIZA MRADI WA MKOMBOZI – MWANAHARAKATI MZALENDO

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, amewataka wakandarasi wanaojenga mradi wa Umwagiliaji Skimu ya Mkombazi, Mkoani Iringa, kuongeza kasi katika ujenzi wa miradi hiyo. Mndolwa amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali unaleta matokeo chanya kwa wakulima katika msimu ujao, na kuagiza wakandarasi kumaliza kazi hiyo hadi mwishoni mwa Oktoba mwaka huu.

Katika kikao kazi kilichofanyika mkoani humo, Mndolwa aliwaagiza wakandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati. Mradi wa Mkombozi, unaojengwa na kampuni ya ndani ya Cimfix & Engineering kwa ajili ya Lot I na II, pamoja na kampuni ya CRJE Engineering kutoka China kwa Lot III na IV, unatarajiwa kugharimu Shilingi Bilioni 56.

Mkurugenzi Mndolwa pia aliongoza kikao na Mkandarasi M/S Cimfix & Engineering Co Ltd, ambapo alitoa maelekezo kuhusu masuala mbalimbali ili kuboresha matokeo ya mradi. Alisisitiza kuhusu mabadiliko katika usanifu wa mfereji, kuongeza urefu wa gabions, kuweka guardrails, na kujenga kibanda kwenye jiwe la msingi ili kuhakikisha miundombinu inalindwa kutokana na mafuriko.

Katika ukaguzi wa miradi ya Lot I na II, maagizo maalum yalitolewa, ikiwemo kurudisha mto katika mkondo wake wa asili na kubadilisha mfereji wa wazi kuwa uliofunikwa. Timu ya wataalam wa Tume itaanza kazi tarehe 09/09/2024 ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande mwingine, Mndolwa alizungumza na viongozi wa Kampuni ya CRJE, akikazia umuhimu wa kuongeza kasi katika ujenzi wa mradi wa Mkombozi. Alisisitiza utambuzi na upimaji wa shamba la Mkombozi ili kusiwe na vikwazo vya kikamilisha miradi hiyo. Meneja wa Mradi, Peter Akonaay, alisisitiza umuhimu wa kushughulikia masuala ya kiufundi yaliyojadiliwa na kumhimiza mkandarasi kuyachukulia kwa umakini mkubwa.

Mkurugenzi wa CRJE, Zhang Lin Jie, alikiri kupokea maagizo hayo na kusema kampuni yake itapanga rasilimali na vifaa vinavyohitajika ili kufikia lengo la ukamilishaji kwa angalau 95% ifikapo tarehe 30 Oktoba, 2024.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts