Dar es Salaam. Wanafunzi 17 wamefariki dunia na 14 kujeruhiwa katika ajali ya moto iliyotokea katika Shule ya Msingi ya Hillside Endarasha iliyopo nchini Kenya.
Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Nation, tukio hilo limetokea usiku wa Alhamisi Septemba 5, 2024 na kuteketeza baadhi ya mabweni ya shule hiyo.
Msemaji wa polisi nchini humo, Dk Resila Onyango, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyokatisha uhai wa wanafunzi hao na kuwa chanzo chake hakijajulikana.
Dk Onyango amesema wanafunzi 16 wamefariki hapohapo katika eneo la tukio na mmoja alipoteza uhai wakati akipatiwa matibabu.
“Miili ya wanafunzi 16 waliofariki katika eneo la ajali imeteketea kiasi cha kutotambulika,” amesema Dk Onyango wakati akizungumza na Nation FM.
Kuna hofu kwamba idadi ya waliokufa katika ajali hiyo inaweza kuongezeka kadiri shughuli ya uchunguzi na uokozi inavyoendelea.
Tayari timu ya uchunguzi imeshafika katika eneo hilo ili kutafuta chanzo cha tukio hilo ili hatua zingine ziweze kufuatawa.
Kupitia mtandao wa X, Rais wa nchi hiyo William Ruto ametoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza watoto wao huku akiwaombea majeruhi kupona kwa haraka.
Pia ameagiza mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Shirika la Msalaba Mwekundu nchini humo kupitia mtandao wa X, limesema litaendelea kutoa huduma za msaada wa kisaikolojia kwa wanafunzi, walimu na familia zilizoathirika na limeanzisha dawati la ufuatiliaji katika shule hiyo.
Imeandaliwa na Mariam Mbwana kwa msaada wa mtandao