Nondo nne za Boka Yanga

MASHABIKI wa Yanga wanachekelea kiwango cha beki mpya wa kushoto, Chadrack Boka aliyeanza kazi kibabe ndani ya mechi nne tu,lakini makocha nao wakafunguka namna timu hiyo ilivyoteseka kwa miaka 10 kupata mtu wa namna yake.

Tangu Yanga iwe na beki wa kushoto Mrundi mwenye asili ya DR Congo Ramadhan Wasso, timu hiyo haikuwahi kupata tena beki wa namna hiyo hadi sasa akashushwa Boka.

Boka amerudisha utamu katika beki wa upande huo ndani ya Yanga ambapo amewatoa mashaka mashabiki wa Yanga ambao walikuwa na wasiwasi tangu kuondoka kwa Joyce Lomalisa.

Vigogo wa Yanga walikuwa wanaona Lomalisa anapungua ubora, ambapo beki huyo mkongwe, licha ya kucheza mechi nyingi msimu uliopita uliokuwa wa mwisho kwake, alitoa asisti mbili pekee msimu mzima wa Ligi Kuu Bara akizidiwa na Nickson Kibabage aliyekuwa na asisti nne, huku akicheza mechi chache.

Takwimu hizo ukiongeza na majeraha ya mara kwa mara makocha wa Yanga na hata mabosi wa Yanga kuanza mchakato wa haraka kusaka beki mpya wa upande huo. Yanga imekuwa na mabadiliko makubwa wa upande wa kushoto ambapo walikuwa wanakosa kupata mtu kama Wasso au Boka. Kuna nondo nne zinazombeba kiufundi eneo hilo;

Jukumu la kwanza kwa beki yeyote ni ulinzi ambalo Boka ndani ya mechi nne licha ya timu hiyo kuruhusu bao moja kwenye mchezo wa ngao ya jamii dhidi ya Azam, lakini hana lawama kwa kuwa alifanya na alitimiza sawasawa majukumu hayo.

Kama kuna kitu kimempa heshima Boka ndani ya Yanga tangu aanze kuichezea timu hiyo ni namna alivyomkimbiza beki wa kulia wa Azam, Lusajo Mwaikenda katika mchezo huo huo ambao Yanga ilipindua meza na kushinda kwa mabao 4-1 wakitokea nyuma.

Boka alimkimbiza beki huyo na kwenda kupiga krosi kali ambayo ikamkuta beki wa kati wa Azam Yoro Diaby na kuuweka wavuni kwake Yanga ikirudisha bao, lakini beki huyo amekuwa akipandisha mashambulizi kwa nguvu na kupiga krosi nyingi kali na kurudi haraka kuzuia.

Endapo Yanga ikikosa kabisa beki wa kati, Boka anaweza ‘kuzima’ hapo na mambo yakaenda sawa kama ambavyo alifanya hivyo juzi kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Kiluvya United ambao timu hiyo ilishinda kwa mabao 3-0 akiwa pia amewahi kucheza mechi moja akiwa na timu yake ya zamani ya FC Lupopo akicheza mechi moja eneo hilo.

Boka ana kimo kirefu ambapo ndani ya Yanga amekuwa ameanza kupewa jukumu la kuhakikisha kwa mipira ya juu kama sio yeye basi Ibrahim Hamad ‘Bacca’ mmoja wao lazima atangulie kugusa mpira kwa kuokoa wakati timu hiyo inashambuliwa kwenye adhabu ndogo au kona.

Wakati Yanga inaanza msako wa beki wa kushoto, watu wasichofahamu nusura mabosi wa timu hiyo watue kwa Valentin Nouma ambaye sasa yuko Simba.

Iko hivi Boka na Nouma wote walikuwa FC Lupopo wakicheza nafasi moja lakini Boka ndiye aliyekuwa anapata nafasi kubwa ya kuanza kama chaguo la kwanza.

Wakati Yanga ikisaka beki wa kushoto wakaletewa jina la Nouma na kuanza kujipanga na ghafla wakapenyezewa taarifa kwamba kama wanataka beki wa kushoto basi wakamchukue Boka na mabosi wa timu hiyo wakajikuta wako njia panda wakamchukue yupi.

Akili ambayo Yanga iliitumia ni Rais wao injinia Hersi Said akasafiri kwa siri mpaka Congo kwenda kujionea mwenyewe Boka ni wa aina gani ambapo bosi huyo akakubali mziki wa beki huyo.

Wakati Yanga inajiridhisha juu ya Boka, akatokea Bilionea wa TP Mazembe Moise Katumbi ambaye alikutana pia na Hersi kisha akamwambia kama timu yake inataka beki wa kushoto basi ni Boka ambaye hata yeye alikuwa anamtamani lakini akashindwa kumsajili kutokana na Lupopo ambao ni wapinzani wake wa jadi wasingeweza kumuuzia kwa gharama yoyote.

Kocha Papy Kimoto wa Union Maniema ameliambia Mwanaspoti mabeki wenye ubora kama wa Boka huwa hawaji mara kwa mara na kwamba Yanga ilifanya maamuzi sahihi ya kumchukua akisema atawabeba.

“Boka ni beki bora sana kwa wachezaji wakongomani wanaocheza hapa Afrika, najua yupo Yanga walifanya usajili mzuri, sio rahisi kuwa na mabeki kama huyo anakaba anashambulia kwa uwiano uleule na akawa na kimo kama chake,”alisema Kimoto.

Kocha wa zamani wa Yanga, Raul Shungu alisema Yanga ilifanya maamuzi sahihi kuachana na Lomalisa na kumchukua Boka ambaye bado umri wake unamruhusu kutumika kwa nguvu akijua kukaba na kushambulia.

“Lomalisa huwezi kumlinganisha na Boka, hawa wote ni vijana wangu, Lomalisa alikuwa hatari miaka ya nyuma, Yanga kumchukua Boka yalikuwa maamuzi sahihi zaidi, atawasaidia kwa muda mrefu kwa kuwa bado ni kijana ana nguvu, kama mnavyomuona anakaba vizuri na anashambulia,”alisema Shungu ambaye amewahi kuifundisha Yanga kwa mafanikio.

Related Posts