Simba yatisha Waarabu | Mwanaspoti

JOTO la Simba limeanza kuwaingia Al Ahly Tripoli ya Libya baada ya kuitana mezani kuweka yamini jinsi ya kuwakabili wawakilishi hao wa Tanzania kwenye mechi mbili za Kombe la Shirikisho.

Wamempa masharti mazito, Kocha Mtunisia Chokri Khatoui kwamba lazima kwa namna yoyote timu yao ivuke sambamba na kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja wenye sharti la lazima wafanye vizuri Caf.

Simba itaanzia ugenini Septemba 15, saa 2 usiku na Mwanaspoti linajua wiki hii watatangulia vigogo wawili kuweka mambo sawa.

Simba inaendelea kujifua kwa ajili ya mechi hizo za kimataifa huku kocha Fadlu Davids akijipa wiki mbili za aina yake ndani ya Septemba kujipanga mapema ili kuwapa raha mashabiki wa Msimbazi.

Simba iliyoanzia raundi ya pili ya michuano hiyo ya CAF, imepangwa kukutana na Al Ahli ya Libya iliyoing’oa Uhamiaji ya Zanzibar, huku mabosi wa timu hiyo wakianza mikakati mapema.

Jambo la kwanza ambalo mabosi wa Simba wameanza nalo, ni kuhakikisha kwanza watangulizi wanawahi ugenini siku yoyote wikiendi hii, wachezaji wote wanapata visa kwa wakati ya kwenda Libya, huku wakitambua wana wiki mbili ngumu kwao na badae wakirudiana jijini Dar es Salaam Septemba 22.

Mbali na hesabu hizo, kocha Davids wa timu hiyo anakabiliwa na mechi nyingine mbili ngumu za Ligi Kuu zitakazotaka kuendeleza rekodi ya ushindi kwa asilimia 100, hivyo baada ya Al Ahli Tripoli itamenyana dhidi ya Azam FC Septemba 26 Kwa Mkapa. Kisha wataifuata Dodoma Jiji katika mchezo mwingine wa Ligi utakaopigwa Septemba 29, Uwanja wa Jamhuri na kuhitimisha wiki mbili za kibabe.

Katika kuhakikisha Simba inafanya vizuri kocha Fadlu aliwaomba viongozi kupata michezo angalau miwili ya kirafiki ili kujiweka fiti kwenye kipindi hiki cha mapumziko kupisha kalenda ya mechi za kimataifa za FIFA.

Viongozi wa timu hiyo wakakubaliana na matakwa ya kocha huyo na kikosi hicho kikacheza na Al Hilal ya Sudan wiki iliyopita na kutoka sare ya 1-1 baada ya hapo kesho Jumamosi kitacheza mechi nyingine ya pili ya kirafiki dhidi ya maafande wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa KMC.

Baada ya mchezo na Al Hilal, Fadlu aliweka wazi kwamba mechi hiyo kwao ilikuwa kipimo sahihi kwao kwani baadhi ya nyota ambao walikuwa majeruhi walipata nafasi ya kucheza na kurejesha utimamu wa kimwili vizuri jambo ambalo limekuwa na tija.

“Joshua Mutale na Chamou Karaboue walipata majeraha ila tunashukuru wamerejea katika kipindi kizuri ambacho tunawahitaji kwa pamoja, michezo hii miwili ya kirafiki tunaitumia kwa ajili ya kutoa nafasi kwa kila mmoja wetu kikosini,” alisema Fadlu aliyeiwezesha timu hiyo kushinda mechi mbili mfululizo za Ligi.

Simba ilianza kwa kuifunga Tabora United kwa mabao 3-0 kisha kuichapa Fountain Gate kwa mabao 4-0 na kuifanya iongoze msimamo kwa pointi sita kama Singida Black Stars, lakini ikibebwa na mabao ya kufunga na kufungwa, kwani yenyewe imefunga saba na kutoruhusu nyavu zao kuguswa hata mara moja.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema, wao kama viongozi hawana haraka ya kwenda Libya mapema kwa ajili ya mchezo huo kwa sababu wanawatambua vyema wapinzani wao, ingawa wataenda kuanzia kati ya Septemba 10 hadi 12.

Simba iliyoanzia raundi ya pili katika mashindano hayo, inakutana na Al Ahli Tripoli iliyofuzu hatua hiyo kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-1 dhidi ya Uhamiaji baada ya kushinda 2-0 kisha 3-1 mechi zote zikipigwa jijini Tripoli Libya baada ya Uhamiaji kuchagua kucheza mechi ya nyumbani ikiwa huko.

BEKI wa kati wa Simba, Hussein Kazi, amesema anaendelea kupambana kupata nafasi ya kucheza kikosini, akizingatia ukweli kwamba mchezaji yeyote anayekosa nafasi chini ya kocha Davis Fadlu anapaswa kulaumu bidii yake mwenyewe.

Kulingana na Kazi, kocha huyo anataka kila mchezaji afanye juhudi za kuimarisha kiwango chake bila kusukumwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kazi alieleza kocha Fadlu ni muwazi kuhusu madhaifu ya wachezaji na huwataka kuyafanyia kazi ili wawe na mchango mkubwa kwa timu kwenye mechi mbalimbali za mashindano. Kocha huyo hurudia kusisitiza hili, na anapoona mchezaji hafanyi bidii, huonekana kama mchezaji huyo ana mzaha.

“Kocha Fadlu mara kwa mara hutukumbusha kwamba tuko Simba kwa ajili ya kufanya kazi na kufanikisha malengo ya klabu. Kwa hiyo, kila mmoja wetu analazimika kupambana katika nafasi yake, hali ambayo inafanya iwe vigumu kwa mchezaji kuzembea mazoezini,” alisema Kazi.

Aliongeza kwa kusema; “Chini ya Kocha Fadlu, nimejijengea kujiamini zaidi, kwani anatuambia mara kwa mara kwamba tusipojiamini sisi wenyewe, hakuna mtu mwingine atakayebeba jukumu hilo la kutufanya tujiamini.”

Kwa mujibu wa Kazi, ameanza kujifunza zaidi kwa kuwaangalia mabeki wengine wanaocheza nafasi yake ili kuongeza maarifa na ustadi wake wa kiufundi, jambo litakalomsaidia kuwa bora zaidi pindi atakapopata nafasi ya kucheza.

Kazi alipoulizwa kuhusu kiwango cha wenzake wanaocheza nafasi moja naye, akiwemo Che Fondoh Malone, Abdulrazack Hamza na Karaboue Chamou, alijibu kwamba wote ni wachezaji wazuri ambao wanamhamasisha ajitume zaidi.

“Kocha ndiye anayejua nani aanze katika kila mechi, kwani kila mchezo una mipango yake. Ninaupenda ushindani huu kwa sababu unanijenga zaidi na kunifanya niendelee kupambana siku hadi siku,” alihitimisha Kazi, ambaye huu ni msimu wake wa pili akiwa na Simba baada ya kujiunga akitokea Geita Gold.

Related Posts