SULUHU YA KISIASA INAHITAJIKA – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyassa, Mchungaji Peter Msigwa, amejibu hadharani madai ya mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, kuhusu kashfa dhidi yake. Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Msigwa ameonekana kushikilia msimamo wake huku akisisitiza kuwa mgogoro huu unahitaji kutatuliwa kisiasa.

Msigwa ameandika, “Kumbe mwamba huwa ananifuatilia. Si walisema nipuuzwe? Niliomba hoja zangu zijibiwe, na baadhi ya viongozi wandamizi wa CHADEMA wamesisitiza hoja zangu zijibiwe.” Kauli hii inaashiria kuwa Msigwa anahisi hoja zake zimepuuzwa ndani ya chama cha zamani alichohama.

Aidha, Msigwa alimshauri Mbowe kwamba tatizo hili linaweza kutatuliwa kisiasa badala ya kuacha hali hiyo kufikishwa mahakamani. “Freeman (Mbowe), wacha nikukumbushe kirafiki, ‘tatizo la kisiasa linahitaji suluhu ya kisiasa’. Nitaacha hakimu aamue,” aliandika Msigwa, akiashiria kuwa hatapambana kisheria pekee bali anataka masuala ya kisiasa yazungumziwe kwa mapana zaidi.

Kauli hizi zinajiri siku chache baada ya Mbowe kumtaka Msigwa kuomba radhi na kulipa fidia ya shilingi bilioni tano (5,000,000,000/=) kufuatia madai ya kumkashifu hadharani. Hii ni baada ya Msigwa kudai kuwa Mbowe Foundation inahusishwa na kuendesha CHADEMA, pamoja na kumhusisha Mbowe na mali binafsi kama helkopta na msafara wa magari zaidi ya kumi, madai ambayo Mbowe ameyataja kuwa ya uongo na yenye nia ya kumchafua.

Hadi sasa, bado haijajulikana iwapo Msigwa atafuata wito wa kuomba msamaha kama ilivyotakiwa na mawakili wa Mbowe, au kama kesi hiyo itachukua mwelekeo wa kisheria.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts