Morogoro. Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema michezo imekuwa ikisaidia kudhibiti vitendo vya uhalifu, ujambazi na utumiaji wa dawa za kulevya na hivyo ameagiza kuimarishwa kwa timu za majeshi kwa kuhusisha timu mbalimbali.
Akifungua michezo ya majeshi inayofanyika Morogoro kuanzia Septemba 6 hadi 15, Makamu huyo wa Rais amesema kufanyika kwa michezo hiyo ni utekelezaji wa sera ya majeshi, lakini hufanyika kwa ajili ya kuimarisha afya na kuongeza wigo wa ajira.
“Tutumie michezo hii kama kipimo cha nidhamu, kama majeshi kwa kutambua kuwa kuna maisha baada ya kazi, lakini pia michezo inajenga afya na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza kikiwemo kisukari,” amesema makamu huyo wa pili wa Rais Zanzibar.
Awali, akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais, Mnadhimu Mkuu wa Majeshi, Luteni Jenerali Salum Hajji Othuman amesema kuwa michezo imeandaliwa na vyombo vya ulinzi na usalama na idara maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya usimamizi wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (Bamata).
Amesema majeshi ni mihimili mikuu ya nchi siyo tu katika masuala ya ulinzi na usalama, bali michezo kwa kuwa huimarisha afya za wanajeshi, hukuza uelewano na ushirikiano miongoni mwao sambamba na sekta ya michezo kwa kutoa burudani.
Luteni Jenerali Jenerali Othuman amesema kwa mujibu wa sera ya maendeleo ya michezo ya Taifa, wakati wa amani wana nafasi nzuri ya kuwashirikisha wanajeshi katika michezo ili kujenga afya ya miili, akili na kuwaleta pamoja kufahamiana.
“Kwa kuwa vijana wengi ni askari wenye uwezo mkubwa wa kuliwakilisha Taifa katika michezo ya mashindano ya kimataifa, tumedhamiria kuikuza na kuiendeleza sekta ya michezo nchini kupitia kwenye majeshi kama ilivyokuwa miaka ya zamani ambapo timu zetu za majeshi, wanamichezo wanajeshi na mshiriki mmoja mmoja walitoa uwakilishi bora kwa nchi katika mashindano ya kimataifa,” amesema Luteni Jenerali Othuman.
Akitoa taarifa taarifa za michezo hiyo, Mwenyekiti wa Bamata, Brigedia Jenerali Said Hamis Said amesema mashindano hayo yana lengo la kuwakutanisha wanajeshi wa majeshi yote nchini ili kuboresha afya.
Amesema mashindano hayo yanashirikisha kanda saba za majeshi ambazo ni Jeshi la Ulinzi wa Wananchi, JKT, Polisi, Magereza, Uhamiaji, zimamoto na Uokoaji pamoja na Idara Maalumu za SMZ.
Ameongeza kuwa mashindano hayo yanatafanyika katika viwanja vya Jamhuri, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), kampasi ya Edward Moringe Sokoine, Viwanja vya JKT Umwema huku mchezo wa shabaha ukitarajiwa kufanyika katika uwanja maalumu wa jeshi uliopo kambi ya Pangawe.
Kwa upande wake, Kanali Martin Sumari ambaye ni katibu wa Bamita amesema mashindano yatahusisha michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu, netiboli, wavu, riadha, masumbwi, shabaha na mishale.