Unguja. Baada ya Chama cha ACT-Wazalendo kutangaza baraza kivuli la wasemaji wa wizara 16 Zanzibar, kati yao nafasi ya usemaji mwanamke ikiwa moja, wanaharakati na wadau wamekishauri chama hicho kurejea upya uteuzi huo ili kizingatia usawa wa kijinsia.
Katika baraza hilo lililotangazwa Septemba 6, 2024, wizara moja ya Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalumu ndiyo yenye msemaji mwanamke, ingawa ujumla kuna wizara 10 zenye naibu wasemaji wanawake.
Wakizungumza na Mwananchi kuhusu uteuzi huo, wadau wa masuala kijinsia wamesema chama hicho ni kikubwa, hivyo kimetoa mwelekeo wake iwapo kitashika dola, namna ambavyo kinaweza kisizingatie masuala ya kijinsia katika dunia ya sasa ambayo inataka asilimia 50 kwa 50.
Mkurugenzi wa Chama cha Wanawake Wanasheria Zanzibar (Zafela), Jamila Mohamed amesema inasikitisha jambo hilo kutokea siku chache baada ya kumaliza programu maalumu iliyovihusisha vyama vya siasa, kuhusu masuala ya kijinsia na chama hicho kilieleza kilivyo na sera ya wanawake.
“Chama hiki kwanza kina sera ya wanawake, sisi tulidhani kiwe ndiyo champion (kinara) wa kuzingatia masuala haya, lakini kilichofanyika kinasikitisha kwa kweli,” amesema Jamila.
Jamila amesema wamekuwa wakihamasisha sera ya jinsia na wao wameshaipitisha.
“Sasa kama wana sera lakini wanakuja na baraza halina uhalisia, tulitegemea wenyewe wawe ni mfano maana hata CCM (Chama cha Mapinduzi) hawajawa na sera ya jinsia,” amesema.
Kwa mujibu wa Jamila, chama hicho kimetengeneza mwongozo kama geresha, hakiufuati.
Amesema ili kuepuka masuala hayo yasiwe yanajitokeza kwa vyama vya siasa kuwa na mihemko na utashi, ni vyema kufanywa marekebisho ya sheria ya uchaguzi na ya vyama vya siasa, ambazo zitakuwa zinatoa mwongozo moja kwa moja wa kufuata masuala ya usawa wa kijinsia.
“Kama sheria ikitamka kwamba lazima kuwe na jinsia, chama kitakuwa hakina namna, lakini hata Tume ya Uchaguzi iwe na sheria yake, licha ya kwamba wanayo sera ya jinsia,” amesema.
“Kubwa zaidi ni marekebisho ya katiba ambayo kila mmoja kwenye vyama ayazingatie,” ameongeza.
Amesema kigezo kikubwa ambacho kinatumika kwenye vyama vya siasa ni kuona labda wanawake uwezo wao ni mdogo.
“Bado mfumo dume unatawala na wale wanawake waliosoma wanawekwa pembeni, wanawekwa wenye uwezo kiasi, kwa hiyo ikitokea nafasi hawazingatiwi kwa sababu wanaleta kigezo cha uwezo mdogo,” amesema.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa-ZNZ), Dk Mzuri Issa naye amekosoa, akisema ipo haja chama hicho kikajitafakari upya na kurejea uteuzi wake kwa kuwa hakijachelewa.
Amesema ACT ni moja ya vyama vya siasa ambavyo vimekuwa mstari wa mbele kuzungumza masuala ya wanawake, kwa kuwa kina sera ya wanawake lakini katika hilo kinastahili kubadilisha mtazamo wake.
“Tungewashauri wakapitia tena list (orodha) yao, kuweka naibu tu haiwapi nguvu wanawake, kuwapa nguvu ni kuwapa uwaziri (vivuli) kamili,” amesema.
Amesema kwa sasa kuna matamko mengi ya kikanda na dunia yanayotaka masuala ya kijinsia yazingatiwe, wanawake wapewe nafasi kwani inawasadia kuzungumzia matatizo yao na jamii kwa mtazamo wa kijinsia.
“Kwa sababu mkiwepo kwenye meza kama mwanamke hayupo, hata mambo yao hayazungumzwi,” amesema.
Amesema kuna sifa ambazo wanawake wanakuwa nazo ambazo mara nyingi wanaume wanazikosa, ikiwa ni pamoja na ushirikishaji, kujitoa na busara, hivyo siyo rahisi kuwakuta wanawake wanafanya hata ubadhirifu kwani wanajiuliza mara mbili kwa kuogopa.
‘’Hii inaweza kuleta picha kamili ya tunakokwenda kwa sababu hiki ni chama kikubwa kinaweza kushika dola, kwa hiyo kama kikishika dola tunaweza kuwa na hofu kuzikosa nafasi hizo.Tunawaomba waangalie tena nafasi hizi na kujitahidi kufikia usawa wa kijinsia, wanaweza, hawajachelewa na hili linawezekana,” amesema.
Amesema wakifanya hivyo halitakuwa jambo jipya kwani iliwahi kutokea katika Wizara ya Kazi kipindi cha nyuma ambapo iliteuliwa bodi ya ushauri kwa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) wote wakiwa wanaume, lakini baada ya kuonekana kasoro hizo, bodi hiyo ilibadilishwa na kuwekwa wanawake wawili.
Mchambuzi wa siasa na mwanaharakati, Ali Makame amesema hatua hiyo imeonyesha uhalisia wa chama hicho, licha ya kujipambanua kuwa na usawa wa kijinsia lakini ni wa maneno siyo vitendo.
“Hata ukiangalia safu ya viongozi wakuu, wengi ni wanaume.Ipo haja kubadilika, wanawake wanatumiwa mstari wa mbele kuhamasisha masuala ya siasa na mikutano lakini linapokuja suala lenye fursa wanawekwa pembeni, wanapaswa kupewa fursa wasibaki tu kuhamasisha pekee,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu jambo hilo wakati akitangaza baraza hilo, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Othman Masoud alisema wanazingatia usawa kijinsia ndiyo maana hata Kiongozi wa chama ni mwanamke (Dorothy Semu), lakini kubwa zaidi wanaangalia ufanisi.
Alisema katika baraza hilo kivuli zipo nafasi nyingi za naibu wasemaji wanawake, huku Wizara ya Maendeleo ya Jamii wasemaji wake wote wakiwa wanawake.
Alipoulizwa Kiongozi wa Chama hicho, Doroth Semu amesema wanatambua umuhimu wa wanawake na ndio maana wametengeneza sera inayowahusu, hivyo wataendelea kuboresha zaidi kwa kuwajengea uwezo na kuwapika wanawake hususani vijana washike nafasi hizo.
Amesema katika nafasi hizo za baraza hilo kivuli lenye wajumbe 32 kuna nafasi 10 za wanawake ambao ni sawa na asilimia 31.
“Huu ndio mwanzo tutaendelea kuboresha kwa kuwapika wanawake waive waweze kushika nafasi hizi,” amesema.