Dar/Mikoani. Ikiwa ni wiki moja tangu kumalizika Wiki ya Usalama Barabarani, ajali tatu zimetokea katika mikoa ya Mbeya na Morogoro na kusababisha vifo vya watu 25 na majeruhi 77.
Wiki ya Usalama Barabarani iliyoanza Agosti 26 ilihitimishwa Agosti 30, 2024. Kwa kawaida katika wiki hiyo hufanyika ukaguzi wa vyombo vya moto na hutolewa stika maalumu kuonyesha kuwa vimekaguliwa, pia hutolewa elimu ya usalama barabarani.
Mkoani Morogoro watu wanne wamefariki dunia na wengine 15 wamejeruhiwa baada ya magari matatu kugongana eneo la Mikese, Barabara ya Morogoro – Dar es Salaam, Septemba 6, saa 1.30 usiku.
Tayari miili ya watu wawili imetambuliwa, huku dereva wa basi lililosababisha ajali anashikiliwa na polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 7, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Yohana Mjengi amesema miili iliyotambuliwa ni ya Pius Mkude (25), dereva wa Fuso na mkazi wa Dar es Salaam na Kenneth Sinyinza (49), mwanajeshi mkazi wa Dodoma.
Amesema dereva anayeshikiliwa ni Simon Hassan mkazi wa Kihonda, Morogoro aliyekuwa akiendesha basi la abiria mali ya Kampuni ya Kibasa lililokuwa likitokea Morogoro kwenda Dar es Salaam.
“Dereva wa basi alikiwa akilipita gari jingine bila kuchukua tahadhari, hivyo liligonga gari aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa likiendeshwa na Pius Mkude (marehemu) likitokea Dar es Salaam kuelekea Morogoro na baada ya hapo basi hilo lilipoteza uelekeo na kugonga gari lingine Toyota Wish likiendeshwa na Keneth Sinyinza (marehemu),” amesema.
Kaimu Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Scholastica Ndunga akizungumza na Mwananchi kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo amesema wote waliofariki dunia ni wanaume.
“Awali tulipokea miili ya watu watatu ambao walifariki dunia papo hapo baada ya ajali na majeruhi 16, lakini leo asubuhi (Septemba 7) majeruhi mmoja amefariki hivyo kufanya idadi ya waliokufa katika ajali hiyo kuwa wanne na majeruhi waliopo hapa hospitali ni 15,” amesema.
Ndunga amesema majeruhi 10 ni wanaume, wanne ni wanawake na mmoja ni mtoto na wote wapo kwenye wodi za kawaida.
Akizungumzia ajali hiyo, majeruhi wa ajali hiyo, Ally Kipande amesema alikuwa akitoka Kondoa kwenda Dar es Salaam kwa basi la kampuni ya Kibisa na walipofika Mikese, basi hilo liligongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba vinywaji na baadaye lori liligonga gari dogo aina ya Wish.
“Nilikuwa nakwenda Dar es Salaam kusalimia familia yangu, maana ni muda mrefu nilikuwa sijaenda kuwaona. Namshukuru Mungu kwa kutoka salama kwenye ajali hii, nilishuhudia wenzangu wakitoka wakiwa wamekufa,” amesema.
Amesema ameumia kichwani hivyo anahitaji muda wa kupumzika ili afya yake itengemae.
Majeruhi 32 kati ya 44 katika ajali ya basi la kampuni ya A-N Classic wameruhusiwa kutoka hospitalini, huku wengine 12 wakiendelea kupatiwa matibabu.
Wakati majeruhi hao wakiruhusiwa, watoto wachanga sita waliopoteza wazazi wao katika ajali hiyo wamechukuliwa na ndugu zao.
Ajali hiyo ilitokea alfajiri ya Septemba 6, basi hilo lilipokuwa likitokea Mbeya kuelekea mkoani Tabora lilipopata ajali na kusababisha vifo vya watu 12, akiwamo mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo ya familia, Amduni Nassor aliyekuwa dereva.
Akizungumza leo Septemba 7, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema watoto waliopoteza wazazi katika ajali hiyo wamechukuliwa na ndugu zao waliofika kuchukua miili ya wapendwa wao.
Amesema majeruhi 12 wanaendelea na matibabu tisa katika Hospitali ya Chunya na wengine watatu kati ya watano waliokuwa na hali mbaya zaidi wapo Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Ajali ya basi hilo ilitokea ikiwa ni siku mbili zimepita baada ya nyingine kutokea Septemba 4, katika Kata ya Chimala, wilayani Mbarali mkoani hapa ikihusisha basi la Kampuni ya Shari Line iliyosababisha vifo vya watu tisa na kujeruhi wengine 18.
Makamu wa Rais Dk Philip Mpango leo Septemba 7 alikemea tabia za uzembe na kutozingatia sheria za usalama barabarani ambazo zimesababisha kushamiri kwa ajali mbaya za barabarani zinazogharimu maisha ya wananchi wengi.
Akimwakilisha Raia Samia Suluhu Hassan katika kilele cha maadhimisho ya jubilei ya miaka 50 ya Kanisa la New Life Outreach iliyofanyika katika kanisa hilo Sakina, mkoani Arusha amewataka wakaguzi wa magari wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) na Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani kutimiza wajibu wao ili kudhibiti magari mabovu yasiingie barabarani, kuhakikisha vidhibiti mwendo vinafanya kazi, na kukagua sifa za madereva hasa wa mabasi ya abiria na malori.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Makamu wa Rais, amesema wamiliki wa mabasi na malori wanapaswa kuhakikisha magari yao yanakuwa na madereva walau wawili kwa safari zote ndefu zinazozidi kilomita 300.
Pia ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha alama za tahadhari zinawekwa katika maeneo yote hatarishi ya barabara kuu.
Kwa upande wa wasafiri amewataka kuzingatia kufunga mikanda wakati wote wa safari na kutoa taarifa kwa Kikosi cha Usalama Barabarani pale dereva wa chombo wanachosafiria anapoendesha kwa mwendo mkali kupita kiasi.
Juni 13, 2024 Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25 alizungumzia usalama barabarani akisema takwimu za ajali zitokanazo na vyombo vya moto zinaashiria hatari kubwa ambayo kila mtu anapaswa kuongeza umakini.
“Watanzania wengi bado hatuheshimu sheria za barabarani, hatuna nidhamu na matumizi ya vyombo vya moto na alama za barabarani. Madhara yake tunapoteza nguvu kazi ya nchi yetu kutokana na ajali za barabarani ambazo zinatuondolea watu wanaotegemewa katika jamii zetu, wakati mwingine kwa uzembe unaoweza kuepukika,” alisema.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano (2019 hadi Mei 2024), ajali za barabarani zilikuwa 10,093, vifo vilikuwa 7,639 na majeruhi 12,663 miongoni mwao wakipata ulemavu wa kudumu.
“Hebu fikiria, magari binafsi (ajali 3,250, vifo 2,090, majeruhi 3,177). Hebu fikiria, mabasi (ajali 790, vifo 782, majeruhi 2,508). Hebu fikiria, daladala (ajali 820, vifo 777, majeruhi 1,810). Hebu fikiria, teksi (ajali 93, vifo 97, majeruhi 173). Hebu fikiria, magari ya kukodi (sherehe,
misiba, na shughuli maalumu) – ajali 326, vifo 263, majeruhi 302,” alisema.
Dk Mwigulu alisema, “idadi hii kubwa ya majeruhi na vifo vya watu kutokana na ajali utadhani nchi iko kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Jambo hili halikubaliki.”
Alisema ilivyo wengi huona usumbufu na wakati mwingine mpaka kuweka chuki na uadui wanapokumbushwa kuhusu usalama na Jeshi la Polisi wawapo barabarani.
“Tunavunja sana sheria barabarani, hata magari ya Serikali vivyo hivyo, wakati mwingine tunawagonga waenda kwa miguu. Ni wakati sasa jambo hili kuazimiwa na jamii nzima ya Watanzania kwa kuweka mtazamo wa kuchukia ajali,” alisema.