BEKI wa kati wa Azam FC, Yannick Bangala atakuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki moja baada ya kupata majeraha ya misuli ya paja, ‘Hamstring’, wakati wa mchezo wao wa mwisho wa suluhu baina ya timu hiyo na JKT Tanzania Agosti 28, mwaka huu.
Daktari wa Azam FC, Mbaruku Mlinga, aliliambia Mwanaspoti, Bangala kwa sasa yupo chini ya uangalizi wa jopo la matabibu wao baada ya kufanyiwa tathimini ya kina na kugundulika alipata majeraha hayo na JKT Tanzania, ingawa sio makubwa sana.
“Anaendelea na programu ya mazoezi tiba chini ya wataalamu wetu, Vicent Madege, Chris Nyoni na hali yake kwa ujumla sio mbaya sana kwa sababu tumegundua anaweza akakaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki moja au zaidi ya hapo tu,” alisema.
Mlinga aliongeza, kuna uwezekano kwa nyota huyo akawahi mchezo ujao wa timu hiyo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji utakaopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi Septemba 13, ingawa itategemea na maendeleo yake kwa jumla kikosini.
Nyota huyo aliyejiunga na Azam FC Julai 29, mwaka jana akitokea Yanga, amekuwa panga pangua ndani ya kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, na ametengeneza pacha nzuri ya kujilinda kati yake na Mkolombia, Yeison Fuentes.
Tangu msimu huu umeanza, kikosi hicho kimekuwa kikiundwa na mabeki wa kati Bangala na Fuentes ambao wamecheza michuano mbalimbali kuanzia Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Ligi Kuu Bara chini ya aliyekuwa Kocha, Youssouph Dabo.
Kijumla safu ya kujilinda ya kikosi hicho imeruhusu jumla ya mabao manane ambayo ni sawa na wastani wa kuruhusu mabao mawili katika mashindano mbalimbali msimu huu huku kwa upande wa eneo la washambuliaji likifunga mabao saba hadi sasa.