Unguja. Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) kwa kushirikiana na wakaguzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume (AAKIA), wamekamata mabegi manne yenye dawa za binadamu zisizo salama kwa matumizi.
Dawa hizo ambazo thamani yake haijajulikana wala mmiliki wake, zimesafirishwa kutoka nchini India kwa kutumia Shirika la Ndege la Ethopia.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mzigo huo leo Septemba 7, 2024 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Dawa na Vipodozi, Sabrina Idrissa Ahmada amesema dawa hizo si salama kwa watumiaji kwa kuwa hazijasajiliwa na ZFDA.
“Dawa hizo zilifungashwa katika kifungashio kisicho rasmi kusafirishia dawa. Mwingizaji wa dawa hizo si halali kwa kuwa hajasajiliwa na kufuata taratibu zilizowekwa,” amesema.
Sabrina amezitaja baadhi ya dawa hizo kuwa ni za kutibu saratani, goita, magonjwa ya akili na antibiotiki.
Kwa mujibu wa ZFDA, baada ya kuingia nchini mzigo huo ulishughulikiwa na Wakala wa utoaji mizigo, Nassor Humoud Nassor aliyedai kutokuwa na maelezo ya kutosha ya mmiliki halali wa mzigo huo baada ya kuhojiwa na wakaguzi.
Sabrina amewaomba wadau wakiwemo wa sekta ya afya na vyombo vya habari kushirikiana kuhakikisha elimu na miongozo juu ya usalama wa dawa inafika katika ngazi zote za jamii kwa lengo la kulinda afya za watumiaji.
Kutokana na tukio hilo lililotokea Septemba 5, 2024, ZFDA imeziweka dawa hizo chini ya uangalizi na usimamizi maalumu, ikimtaka wakala huyo kuwasilisha barua kujieleza pamoja na vielelezo vya uingizaji wa dawa hizo ili taratibu nyingine za kisheria ziendelee kuchukuliwa.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Habari wa ZFDA, Amne Issa amesema wanaendelea na uchunguzi kwa kumhoji wakala huyo licha ya kuonyesha kutokutoa ushirikiano, hivyo taarifa kamili kuhusu tukio hilo itatolewa baadaye.