BEKI wa zamani wa Yanga, Djuma Shaban anayekipiga Namungo kwa sasa, ametimka nchini kwenda Ufaransa, huku akifunguka kilichofanya aende huko akiwa amepewa muda wa wiki moja kabla ya kurejea kikosini kuungana na wenzake kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Bara.
Djuma aliyewahi kuitumikia AS Vita ya DR Congo kabla ya kutua Yanga misimu mitatu iliyopita, alisajiliwa na Namungo iliyoanza msimu vibaya msimu wa Ligi Kuu kwa kupoteza mechi mbili za awali dhidi ya Tabora United na Fountain Gate, inakabiliwa na mechi nyingine dhidi ya Dodoma Jiji wiki ijayo.
Hata hivyo, wakati wachezaji wengine ambao hawajaitwa timu za taifa wakiendelea kujifua, Djuma yeye alitimkia Ufaransa ambako alisema ameenda kushughulikia ishu za familia inayoishi huko na kwamba ana wiki moja kabla ya kurejea kuungana na wenzake.
Beki huyo aliyecheza mechi zote mbili za awali ambapo Namungo ilipoteza 2-1 kwa Tabora na kulala tena 2-0 kwa Fountain, aliliambia Mwanaspoti kuwa, familia yake iko Ufaransa hivyo aliomba ruksa ya kwenda kukamilisha mchakato wa vibali ili ihamie huko jumla na kutoka DR Congo ilikokuwa ikiishi awali.
Aidha, alisema mchakato huo hautachukua muda mrefu sana, kwani sio jambo gumu kutokana na ukaribu uliopo kati ya DR Congo na Ufaransa linapokuja suala la uhamisho.
“Nimeitwa na Mamlaka ya Ufaransa kwenda kukamilisha mchakato wa kuihamishia familia yangu huko, japo inaishi huko, ila vibali huwa vinaisha muda. Ni rahisi kwa Wakongo kuhamia Ufaransa, hivyo nitarudi Tanzania mapema kwani timu imenipa wiki moja ili kukamilisha mchakato huo,” alisema Djuma.
Mbali na Djuma mchezaji mwingine wa DR Congo aliyepo nchini ambaye familia yake inaishi Ufaransa ni Fabrice Ngoma ambaye mara kadhaa amekuwa akienda huko kipindi cha mapumziko.