Kenya yatangaza siku tatu za maombolezo vifo vya wanafunzi 17

Nairobi. Rais wa Kenya, William Ruto ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa baada ya wanafunzi 17 wa Shule ya Msingi ya Hillside Endarasha  kufariki katika ajali ya moto iliyotokea katika shule hiyo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Nation tukio hilo lilimetokea Alhamisi usiku baada ya bweni moja kuteketea kwa moto.

Katika siku hizo tatu za maombolezo kuanzia  Jumatatu, Septemba 9, 2024, hadi Jumatano, Septemba 11, bendera ya nchi hiyo na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zitapepea nusu mlingoti katika Ikulu, vituo vyote vya kidiplomasia vya Kenya pamoja na ofisi zote za umma.

Awali baada ya kuripotiwa kutokea kwa tukio hilo Rais Ruto alitoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza watoto wao, huku akiwaombea majeruhi kupona kwa haraka.

Katika hatua nyingine Rais Ruto ameagiza mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na watakaobainika kuhusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria. 

Hata hivyo,  tayari timu ya uchunguzi imeshafika katika eneo hilo na inaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo ili hatua zingine ziweze kufuatwa.

Wakati akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini humo, Dk Resila Onyango alisema tukio hilo pia limesababisha majeraha kwa watoto 14 ambao wamepelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu huku chanzo cha moto huo kikiwa bado hakijajulikana.

Imeandaliwa na Mariam Mbwana kwa msaada wa mtandao

Related Posts