Mbeya. Majeruhi 32 kati ya 44 katika ajali ya basi la kampuni ya A-N Classic wameruhusiwa baada ya kupewa matibabu na afya zao kuridhisha huku wengine 12 wakiendelea kupatiwa matibabu zaidi.
Wakati majeruhi hao wakirudi nyumbani, watoto wachanga waliopoteza wazazi wao katika ajali hiyo nao wamechukuliwa na ndugu zao.
Jana, alfajiri ya Septemba 6, 2024, basi kampuni ya A-N Classic lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea mkoani Tabora lilipata ajali na kusababisha vifo vya watu 12, akiwamo mmiliki wa basi hilo, Amdun Nassor ambaye alikuwa dereva huku wengine zaidi ya 36 wakijeruhiwa.
Akizungumza leo Septemba 7, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema watoto waliopoteza wazazi wao katika ajali hiyo wamechukuliwa na ndugu zao waliofika kubeba miili ya wapendwa wao.
Amesema hadi sasa majeruhi 12 ndiyo wanaendelea na matibabu zaidi ambapo tisa wapo Hospitali ya Chunya na wengine watatu kati ya watano waliokuwa na hali mbaya zaidi wapo Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
“Wale watoto walikuwa chini ya uangalizi wa Serikali ambapo ndugu wa marehemu walipofika kubeba miili waliwachukua pia kurudi nyumbani.
“Hadi sasa majeruhi waliobaki ni 12 ambapo tisa wapo Chunya na watatu kati ya wale watano waliokuwa na hali mbaya wapo bado Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya wakiendelea na matibabu,” amesema Homera.
Amesema hakuna ongezeko la vifo na amewapongeza wataalamu wa afya kwa kazi waliyoifanya hadi sasa, akieleza kuwa Serikali itahakikisha changamoto zinazojitokeza katika miundombinu ya barabara inazifanyia kazi.
Hata hivyo, katika taarifa yake jana Septemba 6, 2024, mkuu huyo wa mkoa alizitaka mamlaka zinazohusika na mambo ya barabarani kukutana haraka kuweka mkakati wa kudhibiti ajali hizo.
Alielekeza Jeshi la Polisi kufanya ukaguzi wa kina kwa magari yote mabovu kuyaondoa barabarani na kutofanya kazi mkoani humo, huku Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) ukiweka mabango makubwa maeneo yenye kona kali.
“Latra wajitathimini kwa kushindwa kudhibiti magari yasiyo na vidhibiti mwendo kwani ajali mbili zilizotokea Mbarali na hapa Luanjiro, mabasi hayakuwa na vidhibiti mwendo, nataka mamlaka zote kukutana haraka kudhibiti ajali hizi,” amesema Homera.