Majeruhi ajali iliyoua 12 Mbeya asimulia

Mbeya. Mmoja wa majeruhi katika ajali ya basi iliyoua watu 12 mkoani Mbeya, Frank Mwakibolwa amesimulia namna ajali hiyo ilivyotokea na kujeruhi watu 44, naye akipoteza fahamu mara moja kabla ya kujikuta yuko hospitali.

Mwakibolwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya baada ya kunusurika kifo kwenye ajali ya basi la kampuni ya A-N Classic iliyoua watu 12 na kujeruhi wengine 44.

Ajali hiyo iliyotokea jana Septemba 6, 2024 katika kijiji cha Luanjiro, Wilaya ya Mbeya, huku watu 12 akiwamo aliyekuwa mmiliki wa basi hilo, Amdun Nassor wakifariki dunia papo hapo huku wengine zaidi ya 36 wakijeruhiwa.

Kati ya majeruhi hao, watano walikuwa katika hali mbaya na kuwahishwa katika hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu zaidi, huku wengine wakipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Chunya na kituo cha Afya cha Chalangwa.

Hata hivyo, hadi sasa imeelezwa majeruhi 32 kati ya 44, wameruhusiwa pamoja na watoto wachanga waliopoteza wazazi wao kwenye ajali hiyo ambao wamechukuliwa na ndugu zao, na wengine 12 wanaendelea na matibabu.

Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 7, 2024 kwa maumivu makali, Mwakibolwa amesema hakujua lolote kama kulitokea ajali kutokana na mazungumzo waliyokuwa wakijadiliana na abiria wenzake.

Amesema safari yake ilikuwa ya kwenda Itumbi katika harakati zake za kibiashara, ambapo alikuwa ateremkie Chunya ili atafute usafiri mwingine wa kuelekea Itumbi.

“Hata sikujua ajali ilivyotokea, nilijitambua baada ya kufika hospitali kule Chunya na baadaye nikaondoka, nimefika njiani kuna mtu mmoja sikumjua haraka akaniombea lifti kwenye coaster.

“Baadaye alijitambulisha ni daktari wa hapa Rufaa na mfukoni nilikuwa na simu, nikamuonesha aifungue awapigie ndugu zangu, akanileta hadi hapa usiku na baadaye fahamu kurejea,” amesema Mwakibolwa.

Mwakibolwa ameongeza kuwa kwa sasa anaona nafuu inapatikana kutokana na huduma wanayotoa madaktari na kwamba wakati anafika aliona idadi ya watu wengi.

Amesema hadi sasa tayari ndugu zake wameshafika kumjulia hali na huduma nyingine huku akitoa shukrani kwa wananchi na wataalamu wa afya namna walivyojitahidi kuwasaidia.

“Usiku wakati nafika, huduma zilichelewa kwa kuwa niliona watu wengi na madaktari wakihangaika kusaidia kadri ya uwezo wao, lakini kwa ujumla huduma zinaridhisha na niwashukuru kila mmoja kwa nafasi yake.

“Ndugu zangu walianza kufika tangu usiku baada ya kupata taarifa, wengine wanaendelea kuja, sikuwa na mtu mwingine kwenye safari yangu zaidi ya wale niliowakuta kwenye gari tukaendelea kuzungumza,” amesema majeruhi huyo.

Related Posts