Dodoma. Miili ya mama Mwamvita Mwakibasi (33) na mtoto wake, Salma Ramadhan (13) imesafirishwa leo Septemba 7, 2024 kwenda Kiteto mkoani Manyara kwa ajili ya maziko
Wawili hao waliuawa usiku wa kumkia jana Septemba 6, 2024 na watu wasiojulikana nyumbani kwao na kubakwa, Mtaa wa Muungano A katika kata ya Mkonze, Wilaya ya Dodoma mkoani Dodoma.
Wawili hao wanatarajiwa kuzikwa leo Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.
Akizungumza nyumbani kwao Mtaa wa Muungano A katika Kata ya Mkonze, diwani wa kata hiyo, David Bochela amewataka wananchi wote kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu na kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kuwa mitaa yao inakuwa salama.
“Polisi kata pamoja na watendaji wa mitaa tumepeana majukumu ya kufanya lakini tunaomba ushirikiano wenu kwa kuwa sisi wenyewe hatuwezi kuifanya mitaa yetu kuwa salama,” amesema.
Amesema wao wameshirikiana na familia katika mahitaji mbalimbali na watazidi kufanya hivyo hadi jambo hilo litakapokuwa limekamilika.
Mchungaji wa Kanisa la Assembilly of God katika Mtaa wa Mkonze, Festo Mahinyila amesema tukio hilo ni la kusikitisha na lenye kuleta taharuki kwa jamii hasa kwa mtaa wao na kwa mkoa kwa ujumla.
“Jambo hili limekuwa ni la kikatili, tunajaribu kutoa rai kwa Serikali kwamba wajaribu kuangalia kwa jicho la tatu, nini kinaendelea na sababu yake ni kitu gani. Kwa pande wetu kama viongozi wa dini, tuchukue hatua ya kumrudia Mungu na kuwaita watu kumrudia Mungu,” amesema.
Sheikh wa Kata ya Mkonze, Jumanne Kisaka amesema msiba huo umetokana na kukosa hofu ya Mungu, jambo ambalo limewapa hofu wakazi wa mtaa huo.
“Tukio hili ni mwendelezo wa matukio ya majonzi yanayoendelea katika nchi hii, sisi kama viongozi hatuna raha katika hili. Tutaswali na tutamuomba Mungu katika kila aina ya maombi, jambo hili liweze kutuepuka,” amesema.
Mmoja wa waombolezaji, Veronica Shedrack amesema mambo hayo yanapotokea katika jamii huleta mtafaruku na kwa Mkoa wa Dodoma hali si shwari kwa sababu wanashuhudia watoto wadogo wakibakwa na wengine kuuawa.
“Kama mama na mtumishi wa umma inauma, binafsi kama mtumishi wa Mungu niombe kuwa tunapaswa kutubu, ukisoma Biblia Sodoma na Gomora iliangamia yote,”amesema.
Amelitaka Kanisa kusimama katika nafasi yake lakini Serikali pia ichukue hatua madhubuti kuhusiana na kuomba kutofumbia macho mambo kama haya ambayo yamekuwa yakisumbua Watanzania.