RC aipa mbinu Mbeya City kurejea Ligi Kuu Bara, awaita wadau

Wakati Mbeya City ikiahidi kurejea Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2025/26, Mkuu wa mkoa huo,  Juma Homera ametangaza mkakati kwa timu hiyo kuhakikisha inshinda mechi za nyumbani na  kuwataka wadau na mashabiki kuungana kwa pamoja ili kufikia malengo.

Mbeya City inajiandaa na Ligi ya Championship kwa msimu wa pili mfululizo na sasa matumaini yao ni kuona timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya ikirejea tena Ligi Kuu msimu wa 2025/26.

Akizungumza leo Septemba 7, kwenye kilele cha Mbeya City Day, Homera amesema mkakati wa sasa ligi itakapoanza ni kuhakikisha mechi zote za nyumbani City inavuna ushindi na siyo kupoteza wala kuruhusu sare.

Amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itakuwa pamoja na timu hiyo kuweka nguvu ndani na nje ya uwanja.

“Naijua sana Championship,  inahitaji umoja na ushirikiano,  wachezaji pambaneni, mechi zote za nyumbani hakuna sare wala kupoteza wakati huohuo za ugenini tutajipanga,” amesema Homera.

Mkuu huyo pia aliupongeza uongozi mpya wa timu hiyo chini ya Mtendaji Mkuu, Ally Nnunduma kwa kuwa anaona uelekeo mzuri katika kufikia malengo na kukata kiu ya mashabiki.

Mtendaji mkuu wa Mbeya City, Nnunduma amesema pamoja na kuunganisha wadau na mashabiki wote kuisapoti City,  lakini uongozi umejipanga kuipandisha tena timu.

Amesema muitikio wa wadau na mashabiki jijini humo unaongeza hamasa kubwa kwa wachezaji na viongozi katika kufikia malengo akiahidi kuwa msimu huu ndio mwisho wa kucheza Championship.

“Tunawashukuru mashabiki na wadau kwa muitikio katika tukio hili la kihistoria, uongozi tutajitahidi kushirikiana nao kwa kuwa timu ni yao, sisi ni watendaji na lengo ni kuona tunarejea Ligi Kuu,” amesema Nnunduma.

Mmoja wa mashabiki wa timu hiyo, George Mwalyanzi amesema ubunifu wa uongozi katika kuandaa tukio la heshima kuwakutanisha wadau na mashabiki ni hatua ya kwanza kutafuta mafanikio mapya.

“Hili tukio tulizoea kuona kwa timu kubwa za Simba na Yanga,  lakini Mbeya City nayo kwa kuona ukubwa wake na heshima ya mashabiki na wadau, viongozi wametuleta karibu, tunaiona Mbeya City mpya yenye malengo msimu huu,” amesema Mwalyanzi.

Related Posts