Simba, Yanga zashusha presha kwa mastaa kimataifa

HAUTOKOSEA ukisema Yanga na Simba zimefanya uamuzi wa kiufundi unaoweza kuwa na faida kwao kwenye mechi za kwanza za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika na zitacheza ugenini mwishoni mwa wiki ijayo.

Ijumaa, Simba itakuwa Libya kuvaana na Al Ahli Tripoli ya huko kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na Jumamosi, Yanga itakuwa Ethiopia kukabiliana na CBE.

Uamuzi huo ni wa kusafirisha moja kwa moja wachezaji wao ambao wapo katika majukumu ya timu zao za taifa kuungana na timu zao moja kwa moja wakitokea katika nchi tofauti ambako timu zao za taifa zilikuwa zinacheza badala ya kurejea hapa nchini.

Hofu ilikuwa kubwa zaidi kwa Yanga ambayo katika mechi hizi za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 imetoa wachezaji 14 wanaochezea timu tofauti za taifa ambazo zote zitacheza mechi za mwisho nje ya Tanzania.

Katika kuepusha kuwachosha wachezaji hao na safari kwa kutoka huko ambako timu zao za taifa zitacheza mechi za kuwania kufuzu Afcon kuja Tanzania na kisha kusafiri tena kwenda Ethiopia, uongozi na benchi la ufundi la timu hiyo wameamua wachezaji 11 kati ya hao 14 wataungana na timu moja kwa moja Ethiopia huku watatu tu ndio wakiungana nayo hapa Dar es Salaam.

“Ratiba sio rafiki hivyo ni wachezaji wawili tu au watatu ndio wataungana na timu Dar es Salaam wakitokea katika majukumu ya timu zao za taifa na kisha kuondoka pamoja lakini wengine wataungana na kikosi hukohuko Ethiopia,” alisema meneja wa Yanga, Walter Harrison.

Ingawa Harrison hakuwa tayari kuanika majina ya wale ambao watajiunga na timu moja kwa moja ikiwa Ethiopia kuna uwezekano mkubwa wachezaji 13 wakaenda moja kwa moja Ethiopia ambao ni saba wanaochezea timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Abuutwalib Mshery, Dickson Job, Nickson Kibabage, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Mudathir Yahya na Clement Mzize, Duke Abuya (Kenya), Prince Dube (Zimbabwe), Djigui Diarra (Mali) na Stephane Aziz Ki (Burkina Faso) na ambao wanaweza kuungana na kikosi hapa Dar es Salaam ni Clatous Chama na Kennedy Musonda walio katika kikosi cha Zambia na Khalid Aucho aliyepo Uganda.

Aucho atamaliza majukumu yake Jumatatu wakati Chama na Musonda ambao Jumanne ndio Zambia itacheza mechi ya mwisho wanaweza kuingia nchini Alfajiri ya Jumatano pasipo kutumia muda mrefu wa safari.

Wachezaji saba wa Taifa Stars, ikiwa watasafiri moja kwa moja kutoka Yamoussokro Ivory Coast hadi Addis Ababa, Ethiopia, watatumia saa sita na dakika tano ila kama watakuja Dar es Salaam na kisha kuunga kwenda Ivory Coast watatumia saa 12:30 wakiwa angani.

Aziz Ki ambaye atakuwa na mechi Bamako, Mali, atatumia saa saba angani kwenda Ethiopia akitokea huko ambako watacheza na Malawi na akija Dar na kwenda Ethiopia atatumia saa 12:50 angani.

Diarra na Abuya wao watatumia saa 6:10 kutokea Johannesburg, Afrika Kusini kuja Dar es Salaam na kisha kuunganisha kwenda Ethiopia lakini kama wakienda moja kwa moja watatumia saa 5:15.

Mwenye urahisi zaidi ni Prince Dube ambaye atatumia saa 2:05 tu kutoka Entebbe Uganda ambako timu yake ya Zimbabwe itacheza na Sierra Leone kwenda Addis Ababa, Ethiopia lakini kama atakuja Dar na kisha kwenda Ethiopia, atatumia saa 4:30.

Simba nayo imepanga nyota wake wanne waliopo katika timu za taifa kuungana moja kwa moja na timu hiyo Libya ambako Ijumaa itacheza na Al Ahli Tripoli ya huko.

Wachezaji watatu wa Simba wako na Taifa Stars huko Ivory Coast, Mohammed Hussein, Edwin Balua na Ally Salim watatumia saa 14:49 angani ikiwa watatokea Yamoussoukro, Ivory Coast kwenda Libya lakini kama watakuja Dar es Salaam na kisha kwenda Tripoli, watatumia saa 22:19 ikiwa ni karibu siku nzima angani.

Ni kama ilivyo kwa kipa Mousa Camara ambaye naye ataungana na wenzake hao watatu kwa vile yeye atakuwa ametoka kuitumikia Guinea dhidi ya Taifa Stars.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema hakuna uwezekano kwa wanne hao kurudi Dar es Salaam kisha kwenda Libya.

“Kwa mazingira yaliyopo, hao wachezaji wataungana na timu kutokea hukohuko kwa vile tukisema warudi hapa wanaweza kupishana na timu ambayo inaweza kusafiri Jumanne au Jumatano,” alisema Rweyemamu.

Baada ya majukumu ya kimataifa, vigogo hivyo vitarudi kuendeleza vita ya Ligi Kuu Bara ndani ya Septemba kila moja ikikabiliwa na mechi mbili.

Yanga iliyocheza mechi moja hadi sasa ikikusanya pointi tatu, ikimalizana na Wahabeshi, itasafiri hadi jijini Mbeya kuvaana na wageni wa Ligi Kuu, KenGold Septemba 25 na siku tano baadae itarudi jijini Dar es Salaam kuikaribisha KMC kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Kwa upande wa Simba ambao ndio vinara wa ligi hiyo ikikusanya pointi sita katika mechi mbili ilizochezwa ikilingana na Singida Black Stars lakini zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, yenye ikimalizana na Walibya Kwa Mkapa Sepetmba 22, itakaa kwa siku nne kabla ya kuvaana na Azam FC uwanjani hapo.

Mnyama akimalizana na Wanalambalamba iliyoanza msimu kwa suluhu na maafande wa JKT Tanzania, atasafiri hadi Dodoma kucheza na Dodoma Jiji Septemba 29.

Baada ya hapo klabu hizo zitacheza tema mechi chache kila moja tarehe za mwanzoni za Oktoba kabla ya kukutana katika Dabi ya Kariakoo itakayopigwa Oktoba 19 Kwa Mkapa kwa msimu huu baada ya msimu uliopita Yanga kutamba nje ndani kwa kuinyoosha Simba kwa jumla ya mabao 7-2.

Yanga ilishinda Dabi ya Kariakoo ya kwanza ya msimu uliopita kwa mabao 5-1 mcezo uliopigwa Novemba 5 mwaka jana na ziliporudiana Aprili 20 mwaka huu ikafa tena 2-1 na juzi kati kwenye mechi za Ngao ya Jamii ikalala tena kwa bao 1-0, hivyo mechi hiyo ya Oktoba 19 itakuwa ni mechi ya kisasi kwa Mnyama.

Bila ya shaka makocha Miguel Gamondi wa Yanga na Fadlu Davids wa Simba wameshaonja joto ya Dabi, hivyo hawatakaa kizembe hiyo Oktoba 19.

Related Posts