SIMBA inatarajiwa kuvaana na Al Ahli Tripoli ya Libya katika mechi za raundi ya pili za michuano hiyo ikianzia ugenini wikiendi ijayo kabla ya kurudiana nao baada jijini Dar es Salaam na mshindi wa jumla ataenda makundi ili kuanza msako wa ubingwa unaoshikiliwa kwa sasa na Zamalek ya Misri.
Mafanikio makubwa kwa Simba kwenye Kombe la Shirikisho ni kufika hatua ya robo fainali msimu wa 2021/2022 ambapo ilitupwa nje na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed ‘MO’ Dewji, juzi ametua nchini kutoka ughaibuni, kisha kuitisha vikao vizito na vigogo wa klabu hiyo kwa ajili ya kusimamia mikakati ya kuelekea michezo miwili ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mo ambaye muda mwingi amekuwa akiishi Dubai, alitua nchini juzi jioni kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuhakikisha timu hiyo inafuzu makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika akishirikiana na mabosi wengine wa timu hiyo.
Kwa mujibu wa chanzo makini kutoka ndani ya Simba ni kwamba Mo alivyotua tu, moja kwa moja alifanya kikao na watu wachache ndani ya uongozi wa timu hiyo kwa ajili ya kuhakikisha wanaweka mikakati sawa.
Baada ya kikao hicho ambacho kilifanyika katika hoteli moja jijini Dar es Salaam, leo bosi huyo atakuwa tena na kikao na baadhi ya watu wa Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo kabla keshokutwa hajakutana na benchi la ufundi pamoja na wachezaji wa timu hiyo kujua maandalizi yao na uongozi utoe ahadi zake.
“Mo ametua nchini kwa ajili ya maandalizi ya michezo miwili dhidi ya Tripoli ule wa ugenini na mwingine ambao tutacheza hapa nyumbani. Alipofika alifanya kikao na baadhi ya viongozi na kukubaliana kuwa baadhi ya watu lazima wawahi kwenda Libya,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Hilo tunalifanya kila wakati, lakini lilikuwa linasubiri baraka za Mwenyekiti mwenyewe, baada ya kikoa hicho Jumamosi (leo), atakuwa tena na kikao bado sijafahamu lakini nafikiri ni watu wengi kutoka kwenye bodi watahudhuria kwa ajili ya kupata ripoti ya maandalizi ya michezo hiyo na baada ya hapo atakutana na makocha pamoja na wachezaji Jumatatu kabla timu haijaondoka Jumatano ijayo.”
Hata hivyo, alisema uongozi umeshawaambia wachezaji pamoja na makocha kuwa wanaamini timu hiyo inaweza kufika fainali ya Kombe la Shirikisho msimu huu, kama kila mtu atafanya majukumu yake ipasavyo.
Chanzo hicho kimesema kuwa hadi sasa tajiri huyo kijana Afrika amesharidhishwa na mwenendo mzima wa timu na matokeo ambayo imeyapata kwenye ligi lakini akiamini kuwa juhudi zaidi zinahitajika.
“Kwa sasa Mwenyekiti na viongozi wengine wamesharidhika na mwenendo wa timu na kiwango cha wachezaji, lakini kila mmoja anatakiwa aongeze juhudi zaidi kwenye eneo lake. Tageti yetu msimu huu ni kuona tunafika fainali na ikiwezekana tuchukue Kombe la Shirikisho ambalo linashikiliwa na Zamalek ya nchini Misri,” kilisema chanzo hicho.