Simulizi ya mwaka mmoja kijana aliyeoa wake watatu kwa mpigo

Katavi. Julai 7, 2023, mkazi wa Mtaa wa Kivukoni uliopo katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Athumani Yengayenga (36) aliushangaza ulimwengu kwa kufungua ndoa na wanawake watatu siku moja.

Kijana huyo alifikia uamuzi huo ili kukamilisha sunah ya imani ya Kiislamu ambapo dini hiyo inaruhusu mwanaume kuoa wanawake zaidi ya mmoja.

Athuman Yengayenga alifunga ndoa na Fatma Raphael aliyekuwa na umri wa miaka (30), Mariam Manota (21) na Asha Pius (20). Ndoa hiyo ilifungishwa na Sheikh wa Mkoa wa Katavi, Mashaka Kakulukulu ili kukamilisha malengo ya kijana huyo.

Pamoja na watu wengi kushangaa huku kukiwa na mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kwamba ni kwa namna gani ataweza kuishi na wanawake hao wakati hivi sasa kumekuwa na changamoto ya ndoa hata ya mke mmoja na wengine wanatengana.

Mwaka mmoja na miezi miwili baada ya ndoa hiyo, Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na kijana huyo ambaye anaeleza kisa cha yeye kuamua kuoa wanawake watatu na kuishi nao wote kwa pamoja kwa furaha, amani na upendo.

Athumani ambaye alizaliwa mwaka 1988, anasema alipokuwa na umri wa miaka 18, aliingia kwenye uhusiano na mwanamke mmoja ambaye walikubaliana na wazazi wake kwamba watakuja kuoana, lakini baadaye aliachwa.

Amesema alikuwa akiishi na mwanamke huyo bila kufunga ndoa kwa miadi kwamba wangefunga ndoa.

Hata hivyo, amesema waliachana kutokana na mgogoro waliokuwa nao na hawakujaaliwa kupata mtoto.

“Kwa kweli niliumia sana kwa sababu nilikuwa nampenda lakini aliniacha baada ya maisha kuwa magumu. Basi, nilikaa kwa muda mrefu bila kuwa na mwanamke, nilikuwa naishi mwenyewe, nilikuwa nafikiria nikitaka kufunga ndoa nitafunga na wanawake watatu hadi wanne lakini sio kufunga ndoa na mwanamke mmoja ili kuepusha mateso ambayo niliyapata baada ya kuachwa,” amesema.

Picha ya ndoa ya Athumani Yengayenga (36) akiwa na wake zake watatu.

Ameongeza: “Niliamua kufanya hivyo kwa kuamini kuwa nikiwa na wanawake watatu au wane, hawawezi kuniacha wote, hivyo siwezi kuteseka lakini nilikuwa natimiza sunah ya dini yangu ya Kiislamu ambayo imetuamrisha kuoa  hadi wake wanne.”

Alivyowapata wanawake watatu

Athuman anaeleza kuwa baada ya kukaa muda mrefu aliamua kumtafuta Fatma Raphael, mkazi wa Kigoma ambaye alikuwa naye kwenye uhusiano bila kufunga ndoa na walipata watato wawili, hapo alifanikiwa kujenga nyumba lakini alimweleza anataka kuoa wanawake wengine. Anasema mke wake alikubali, akamtafuta Asha Pius, mkazi wa Sumbawanga aliyekuwa amezaa naye mtoto mmoja. Alipomweleza kusudio lake, alikubali. Na mwisho akamtafuta Mariam Manota, mkazi wa Tabora, alimweleza nia yake ya kumuoa akiwa mke wa tatu, akakubali.

“Baada ya wote kukubali, nikaanza taratibu za kufunga ndoa na namshukuru Mungu, nilifanikiwa kufunga ndoa siku moja na wote   watatu. Ilikuwa kazi ngumu sana kwa jamii kunielewa, wengi walishangaa lakini ndio hivyo Mungu mwema,” amesema.

Athumani amesema baada ya kufunga ndoa, maisha yalikuwa magumu kidogo lakini alikaa na wake zake, wakakubaliana wote kwa pamoja kusaidiana na kuishi kama familia moja. Anamshukuru Mungu wake zake walimwelewa, maisha yakaendelea hadi sasa wanaishi vizuri.

“Tulianza kuishi kwenye nyumba za kupanga na wake zangu wawili kwani mke mkubwa alikuwa anaishi kwenye nyumba yangu niliyokuwa nimejenga kabla sijaona, lakini kingine nilichokifanya nilikaa na kuwaeleza hali ya maisha ilivyo kwenye nyumba za kupanga na nikawataka kila mmoja alete mawazo yake.

“Basi, tuliyaweka pamoja na kuyachambua ili kutengeneza mpango mkakati wa namna ya kuyatekeleza hayo mawazo ikiwa ni pamoja na kutoka kwenye nyumba za kupanga na namna ya kufanikiwa kimaisha,” amesema kijana huyo.

Nyumba aliyofanikiwa kujenga Athumani Yengayenga (36) na wake zake watatu ndani ya mwaka mmoja ikiwa katika Mtaa wa Kivukoni Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi. Picha na Idd Hassan

Amesema wote walitoa mawazo mengi ya biashara, kuwekeza, kujenga nyumba na mambo mengi na wakakubaliana kuanza na wazo la biashara pamoja na kujenga nyumba. Amesema aliwafungulia wake zake biashara ndogondogo

“Kuna ambaye ni fundi cherehani, mwingine nikamfungulia duka na mwingine anafanya biashara ya nafaka (mazao) na kipato kinachopatikana kwa kila mmoja kulingana na biashara yake nakikusanya na kukiweka sehemu moja. Tunajadiliana wote kutekeleza vipaumbele ambavyo tumekubaliana kupitia mawazo tuliyokuwa tumeyatoa na kukubaliana,” amesema.

Amesema kama kuna mmoja wao hakufikia kiwango ambacho walikubaliana au biashara zake haziendi vizuri, basi wanamchangia na kuongeza kiasi kilichokuwa kimepungua na kukamilisha malengo waliyokuwa wamejiwekea.

“Hii imetusaidia sana, tulipata pesa za kununua kiwanja baada ya kuishi kwenye nyumba ya kupanga kwa kipindi cha miezi sita tu na tukaanza ujenzi wa nyumba, namshukuru Mungu hivi sasa nimetoka kwenye nyumba ya kupanga, naishi kwangu na wake zangu wawili.

“Tumeanzisha ujenzi wa nyumba nyingine ili kila mke awe na nyumba yake, na ninaamini hilo tutafanikiwa kwani tunashirikiana kwa pamoja na tunakubaliana kufanya jambo kwa pamoja na biashara zinaendelea kukua siku hadi siku, naishi maisha mazuri yenye furaha, upendo na amani,” amesema Athumani.

Kijana huyo ameeleza kwamba baada ya kufunga ndoa na wake zake, hakuwapangia zamu za kulala kwamba leo nitakuwa kwa mke mkubwa, mdogo au wa kati, bali anachokifanya anaenda pale anapotaka, hiyo imemsaidia kuondoa changamoto mbalimbali zinazojitokeze kwenye ndoa.

“Hata wakipishana wenyewe, hawagombani bali wananiambia halafu mimi nakaa na kila mmoja, nasuluhisha na maisha yanaendelea. Kwa kweli wake zangu ni waelewa sana na wanaheshimiana, wanapenda na wanasaidiana kwa kila jambo linalotokea mbele yao. Kwa hiyo sioni changamoto yeyote kuishi na wanawake wengi,” ameeleza.

Ushauri wake kwa wengine walio kwenye ndoa na wanaotarajia, ni kwamba jambo muhimu ni kuwa waaminifu kwani hilo limemsaidia kuishi na wake zake vizuri, lakini wengi wanashindwa kudumu kwenye ndoa zao kutokana na kutokuwa waaminifu.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu maisha ya ndoa yao, Asha ambaye ni mke wa pili, anasema kabla hajaolewa alikuwa anajua maisha mazuri yanakuwa mtu akiolewa mke mmoja lakini kumbe sio hivyo, wao wapo watatu lakini wanaishi maisha mazuri, wanapendana, wanaheshimiana na kunasaidia.

“Kwa wale ambao walikuwa wanafikiri ilikuwa kiki, niwaambie tu ni kweli tuliolewa wanawake watatu na tunaishi vizuri, hatujamuacha mume wetu, tunampenda na tunamjali na yeye anatujali, anatuthamini na mahitaji yetu anatutimizia kwa wakati.

“Ninachowashauri tu wanawake wenzangu ambao wapo kwenye ndoa, waweheshimu wanaume wao na wale ambao wanataka kuolewa, wakubali kuolewa hata wengi, kikubwa wapendane na waheshimiane tu,” amesema Asha.

Kwa upande wake, Mariam Manota ambaye ni mke wa tatu, amesema anafurahia maisha ya wake wengi kwani watu wanawashangaa kwa kuwa walifunga ndoa siku moja wanawake watatu lakini kuna wengine wameolewa hadi wanawake sita lakini siku tofauti tofauti na wanaishi vizuri sawa na wao.

“Wanawake wengi ambao wanawaacha waume zao na kuishi maisha yao sio vizuri kwani maisha ya mwanamke asiye na mume hayana heshima kutokana na anaweza kuwa na uhusiano na wanaume wengi na kuzaa kila mtoto na baba yake, jambo ambalo linafanya watoto kutokuwa na maadili mazuri.

“Wanawake ambao hawana wanaume wanaweza kufurahia maisha wakiwa na nguvu lakini watakapofika uzeeni, wanaishia maisha magumu sana, maana hakuna watu wa kuwaangalia wala kuwajali, hivyo nawaomba wanawake wenzangu wadumishe ndoa zao na waweheshimu waume zao ili kutengeneza familia bora ambayo itakuja kuwasaidia wakizeeka,” amesema mwanamke huyo.

Related Posts