KIKOSI cha Taifa Stars kiliondoka nchini leo kwenda Ivory Coast kwa ajili ya mchezo wa pili wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 utakaopigwa keshokutwa dhidi ya Guinea, huku kocha akiamini watafanya vizuri.
Stars itaingia katika mchezo huo wa Kundi H, ikiwa na kumbukumbu ya suluhu nyumbani mbele ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku wenyeji wa mchezo huo, Guinea ikipoteza juzi ugenini kwa kufungwa 1-0 na DR Congo.
Akizungumzia maandalizi kabla ya timu kupaa, kaimu kocha mkuu wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alisema baada ya mchezo dhidi ya Ethiopia walifanya tathimini ya kikosi na kurekebisha upungufu uliojitokeza na sasa wanaenda kupambana kusaka pointi ugenini.
“Kila mmoja wetu yupo tayari kwa changamoto nyingine. Ni mchezo mgumu kwa sababu tunakutana na wapinzani ambao wamepoteza mechi ya kwanza, hivyo haitakuwa rahisi. Shida kubwa kwetu ilikuwa ni umaliziaji na tumefanyia kazi hilo,” alisema.
Nyota wa kikosi hicho, Novatus Dismas alisema jukumu lao ni kuhakikisha wanapambana dhidi ya Guinea na kwamba hawana presha dhidi ya wapinzani wao.
Guinea inayotumia Uwanja wa Charles Konan Banny uliopo mjini Yamoussoukro, Ivory Coast baada ya viwanja vya nchi hiyo kutokidhi vigezo, iko mkiani mwa kundi hilo ikiwa haina pointi, huku DR Congo itakayoifuata Ethiopia inaongoza ikiwa na pointi tatu, ilhali Tanzania na Wahebeshi wakiwa na alama moja kila moja.
Mara ya mwisho kwa Stars na Guinea kukutana ilikuwa katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) 2021, ambapo zilitoka sare ya kufungana mabao 2-2, Januari 27, 2021, huku mabao ya Tanzania yakifungwa na Baraka Majogoro na Edward Manyama. Fainali hizo zilifanyika Cameroon.