VIDEO: Simulizi ya mwanafunzi alivyotumikishwa kingono siku tatu

Moshi. Mwanafunzi wa kidato cha kwanza aliyetoweka kwa siku tatu nyumbani kwao baada ya kuaga kwenda shule (jina limehifadhiwa) katika Kijiji cha Kifuni, kata ya Kibosho Magharibi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro ameeleza alivyotekwa na kutumikishwa kingono kwa siku tatu bila ndugu zake kujua alipo.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 14 anadaiwa kutekwa asubuhi ya Agosti 28, 2024 wakati akiwahi shuleni na mwanaume mmoja kijijini hapo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 48 ambaye alikuwa akimtumikisha kingono.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema zipo hatua za kiuchunguzi zinazoendelea.

“Kosa lililofunguliwa polisi ni kumtorosha mwanafunzi na ikithibitika ni kweli amemuingilia, litakuwa ni kosa la kubaka, hivyo baada ya kukamilisha vielelezo, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani,” amesema Kamanda Maigwa.

Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 7, 2024, mwanafunzi huyo ameeleza kuwa tangu mwanaume huyo alipomteka, alimfungia ndani kwa siku tatu na kumtumikisha kingono asubuhi na jioni huku akishindia maandazi na soda.

Mwanafunzi huyo ameeleza kuwa mwanaume huyo alikuwa akimtumikisha kingono kila siku na anapomaliza haja yake, humfungia ndani kwa kufuli hadi atakaporudi jioni huku akimpa vitisho na kwamba akitoa siri atamuua.

“Agosti 28, 2024, saa 12 asubuhi, nikiwa naenda shule, nilikutana na baba mmoja ambaye alinishika kwa nguvu na kunivutia ndani kwake na kisha kunifungia. Nilimuuliza kwanini unanifungia ndani, akaniambia kaa kimya na ukipiga kelele nitakuua,” amesema.


Simulizi ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza alivyotumikishwa kingono siku tatu

Amesema alipomfungia ndani kwa siku tatu mfululizo bila kutoka nje, alikuwa akimtumikisha kingono asubuhi, jioni na mchana, alikuwa akimletea maandazi na hicho ndiyo kilikuwa chakula chake siku zote alizofingiwa.

“Nilikaa siku tatu ndani sitoki nje, alikuwa ananibaka asubuhi na jioni, akimaliza anaondoka na kufunga milango, anasema nikipiga kelele ataniua,” ameeleza mwanafunzi huyo.

Anasema baada ya kukaa naye siku hizo tatu, kulipigwa mbiu kijijini hapo akitafutwa na baada ya mwanaume huyo kupata taarifa kwamba binti huyo anatafutwa, alimfungulia mlango na kumtaka aondoke aende shule.

“Baada ya mbiu kupigwa ndio akaniachilia akaniambia niende shule, akasema nisiseme kitu chochote na kama nitasema ataniua,” ameeleza mwanafunzi huyo.

Akizungumzia tukio hilo, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, amesema mtoto wake huyo alikuwa akiishi na mama yake mzazi (bibi) na kwamba akiwa kwenye shughuli zake za utafutaji alipata taarifa ya kupotea kwa mtoto wake huyo na ndipo jitihada za kumtafuta zilipoanza.

“Nilipigiwa simu kwamba mtoto wangu ameenda shule lakini hakurudi nyumbani jioni, baada ya kupata hizi taarifa niliwasiliana na ndugu zangu wengine. Tulimtafuta bila mafanikio siku hiyo, baadaye tulitoa taarifa kwenye vyombo husika ikiwemo polisi na ofisi za kata.

“Baadaye tulipiga mbiu kijiji kizima na ndipo tulipobaini kwamba mtoto wangu yupo kwa huyo mwanaume na ndipo tulipochukua hatua za kisheria,” amesema mama huyo.

Related Posts