Viongozi wamuelezea Machumu, afunguka kuhusu hofu yake

Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wa siasa na Serikali wamezungumza namna walivyomfahamu aliyekuwa Mkurugenzi wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu katika hafla ya kumuaga.

Viongozi wa kisiasa waliohudhuria hafla hiyo iliyofanyika jana (Septemba 6, 2024) ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Emmanuel Nchimbi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Chama ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Mbali na kujikuta katika eneo moja tofauti zao za vyama ziliwekwa kando na wote walisalimiana kufanya mazungumzo baina yao, wakimuaga Machumu ambaye alistaafu kuitumikia MCL Agosti 30, 2024.

Katika hafla hiyo, Mbowe ambaye alikuwa wa kwanza kupewa kipaza sauti amesema alimfahamu Machumu akiwa katika mwaka wake wa kwanza kama mtumishi wa Business Times ambapo alimtafuta akiomba mahojiano naye juu ya nafasi ya sekta ya burudani.

“Nashukuru alichukua makala ile na kuandika, hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kuonana na Bakari, tangu hapo tumekuwa marafiki wa katibu, tunazozana wakati mwingine kwa mambo ambayo wote mnayajua na Nchimbi huenda anayajua zaidi lakini pamoja na hayo haikuondoa kuwa sisi ni marafiki,” amesema Mbowe.

Nchimbi ambaye alikuwa wa pili kuzungumza namna alivyomfahamu Machumu kwa mara ya kwanza usiku saa 8 usiku siku nyingi nyuma.

Amesema siku hiyo Machumu akiwa anapita katika moja ya sehemu alisikia milio ya risasi na alimpigia simu Dk Nchimbi ambaye kwa wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya ndani na kumueleza kilichopo.

“Nilimpigia simu IGP hakupatikana, nikampigia Kamanda wa polisi hapatikani, nikampigia dereva wangu hapatikani, nikaona Waziri wa Mambo ya Ndani si mimi acha niende, nikawasha gari nikaenda, siku ile ninachokumbuka ni uchapakazi wake kuwa alikuwepo kazini hadi muda ule,” amesema Nchimbi.

Kwa upande wake, Zitto yeye alikumbuka namna Bunge la tisa lilivyobadili siasa za Tanzania, huku akiyataja magazeti ya The Citizen na Mwananchi yalivyokuwa yakitumika kusukuma ajenda mbalimbali.

“Nilipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, chombo hiki kilishiriki kwa kiasi kikubwa pasipo mfano kuhakikisha kuwa kinaibua masuala ya uwajibikaji ndani ya Bunge, wakati ilipokuwa ngumu kuingiza kwenye shughuli za Bunge tulishirikiana na magazeti ya The Citizen,” amesema Zitto.

Alitolea mfano wa suala la IPTL iliyokuwa ngumu kuripotiwa  katika chombo chochote cha habari lakini Mwananchi ilifanya.

“Nafahamu kuwa mlipata matatizo mengi sana, kwa niaba ya wenzangu naomba radhi lakini hatimaye iliweza kushika kasi na hatua kuchukuliwa na ilikuwa ni jitihada za magazeti haya,” amesema Zitto.

Zitto pia alikiri kuwa miongoni mwa wanasiasa waliomsumbua sana Machumu na alipoona hapati majibu ya kutosha alienda kuishutumu kampuni mbele za umma.

“Napenda nikushukuru sana na nikupongeze na Mungu akusaidie unapokwenda naamini utaendelea kuwa na mchango mkubwa katika kukuza vipaji kwani wengine tumekulia kwenye kalamu, magazeti na vitabu vyenu,” amesema Zitto.

Mbali viongozi wa vyama, Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba amesema zawadi kubwa ambayo Machumu ameiacha ni ripoti ya utendaji wa vyombo vya habari na hali yake kiuchumi ambapo mapendekezo yake mengi yameanza kufanyiwa kazi.

Amesema Machumu anaondoka wakati ambao kuna mageuzi na mabadiliko makubwa ambayo yamefanyika katika sekta ya habari ambayo alikuwa miongoni mwa waliofanya yatokee.

Makoba amesema kustaafu kwa Machumu haimaanishi kuwa amechoka, huku akieleza kuwa kama Serikali itaendelea kumuhitaji ili asaidie nchi kule atakapokuwa kupitia ushauri, maoni na mawazo katika sekta ya habari.

“Imani yetu utaenda kuwa mwalimu mzuri kwa kuwakuza na kuwashauri vijana wengi wa ndani na nje ya nchi hasa katika kukuza sekta hiyo,” amesema Makoba.

Katika hafla hiyo, licha ya sifa nyingi alizomwagiwa, Machumu anakiri kuwa kuna siku alitamani kuacha kazi katikati ya mkutano wa bodi ya wakurugenzi mwaka 2021.

Wakati huo ambapo Ugonjwa wa Virusi vya Korona (Uviko-19) umeingia nchini, baadhi ya wafanyakazi wa Mwananchi walikuwa wakifanyia kazi nyumbani na wengine wakifanyia kazi ofisini huku bodi ya wakurugenzi ikifanya vikao vyake kila baada ya wiki mbili kwa njia ya mtandao.

“Kuna siku nilitaka kuacha kazi katikati ya kikao cha bodi, kilikua kikao kigumu sana, tuliambiwa tuje na mkakati wa kubadili utendaji kazi wa chumba cha habari ndani ya siku saba, bahati nzuri Mungu si Athumani sisi tulikuwa tumeanza mchakato huo miezi mitatu kabla,” amesema Machumu.

Amesema kupewa nafasi ya siku saba kuliwafanya wao kujipanga vyema namna watakavyowasilisha mkakati huo lakini kabla ya kupewa nafasi hiyo alikuwa amewaza kuondoka.

Aidha Machumu anasema hofu kubwa aliyokuwa nayo wakati wa uongozi wake MCL ni kuhisi kuwa Mwananchi itamfia mikononi na anasema hilo lilimnyima usingizi.

Anasema kiu yake ilikuwa ni kuangalia namna ambayo magazeti na matangazo ya kawaida yanaweza kusaidia kuleta kipato cha kusaidia uandishi wa habari kifedha.

Related Posts