Wanawake CCM waguswa matukio ya ulawiti, ubakaji

Dodoma. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama cha Mapinduzi (UWT), Mary Chatanda ameiagiza kamati ya haki na sheria ya jumuiya hiyo, wabunge na wadau wengine kufanya tathimini ya kina ya sababu za kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia nchini licha ya kuwapo adhabu kali.

Chatanda amesema tathimini hiyo ilenge pia kuona kama vifungu vya sheria vinavyohusika na makosa ya ubakaji na ulawiti vinahitaji marekebisho.

Mwenyekiti huyo ameyasema hayo leo Jumamosi Septemba 7, 2024 wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo, ulioenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria.

“Fanyeni tathmini ya kina kuhusiana na sababu za kuongezeka kwa matukio hayo ya ukatili pamoja kuwepo kwa sheria. Lakini pia ilenge kama kuna umuhimu wa kufanyiwa marekebisho basi tuwasilishe mapendekezo hayo serikalini kuipitia au itungwe sheria mahususi ya kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia ili vitendo hivyo vipungue,” amesema.

Amesema kuwa UWT Taifa inasikitishwa na matukio yakiwemo ya hivi karibuni ya mtoto wa miezi sita kulawitiwa na kubakwa na baba yake mzazi, hali iliyosababisha kifo cha mtoto huyo na tukio la kubakwa na kuawa kwa mama na binti yake.

Usiku wa kuamkia jana (Septemba 6, 2024) Mwamvita Mwakibisi (33) na mwanaye Salma Ramadhan (13), waliuawa na kubakwa na watu wasiojulikana nyumbani kwao Mtaa wa Muungano A kata ya Mkonze jijini Dodoma.

“UWT inalaani matukio haya na kuiomba Serikali yetu kuendelea kutafuta mwarobanini wa matukio haya ya kusikitisha. UWT imekuwa mstari wa mbele katika ajenda ya kuhimiza maadili katika jamii na kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake ambapo ni moja ya kipaumbele chake,” amesema.

Amesema chini ya uongozi wake UWT itaendelea kuwaunganisha wanawake wote na kuwa chombo cha kuwatetea wanawake pale haki zao zinapopokonywa.

Pia amewataka kutoa elimu kwa Watanzania nchini juu ya ukatili wa kijinsia na kutofumbia macho vitendo hivyo hata kama vinafanywa na waume zao.

Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo,  Zainab Katimba amesema imeanzishwa kampeni ya msaada wa kisheria chini ya jumuiya hiyo na itaanza kazi katika mikoa 10.

Amesema kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, kamati itatoa msaada wa kisheria katika ofisi za UWT na kuwa watoto, wanawake na wenye mahitaji maalum watakuwa ni walengwa katika kampeni hiyo.

Amesema wameandaa programu maalum ya kuwafikia watoto shuleni ili kuwapa elimu kuhusiana na ukatili wa kijinsia.

Related Posts