Morogoro. Watu wanne wamefariki dunia na wengine 15 wamejeruhiwa baada ya magari matatu likiwemo basi la kampuni ya Kibisa kugongana katika eneo la Mikese, barabara ya Morogoro – Dar es Salaam jana 1:30 usiku.
Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama hakupatikana mara moja, jitihada za kumtafuta zinaendelea.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Kaimu Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Scholastica Ndunga amesema watu waliofariki katika ajali hiyo wote ni wanaume.
“Awali tulipokea miili ya watu watatu ambao walifariki palepale kwenye eneo la ajali na majeruhi 16, lakini leo asubuhi hii, majeruhi mmoja amefariki na hivyo kufanya idadi ya waliokufa katika ajali hiyo kuwa wanne na majeruhi waliopo hapa hospitali ni 15,” amesema Ndunga.
Amesema hadi sasa bado miili hiyo haijatambuliwa majina na imehifadhiwa katika hospitali hiyo, huku majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu na hali zao zimeanza kuimarika.
Ndunga amesema majeruhi hao 10 ni wanaume, wanne ni wanawake na mmoja ni mtoto na wote wapo kwenye wodi za kawaida.
“Marehemu mmoja aliyefia hapa hospitali kabla ya kukata roho, alijaribu kutaja jina lake lakini hatukuweza kulielewa na hatuwezi kulitaja kwa kuwa alikuwa akitaja jina hilo akiwa katika hali mbaya na hivyo matamshi yake hatukuweza kuelewa vizuri jina lake, naamini kupitia vyombo vya habari, ndugu wa marehemu hawa watakuja kuwatambua,” amesema Ndunga.
Akielezea namna ajali hiyo ilivyotokea, mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Ally Kipande amesema alikuwa akisafiri kutoka Kondoa kwenda Dar es Salaam kwa basi la kampuni ya Kibisa na walipofika eneo la Mikese, basi hilo liligongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba vinywaji mbalimbali na baadaye lori hilo kugonga gari dogo aina ya Wish.
Amesema kwa namna alivyoona ajali hiyo ilivyotokea, anaweza kusema chanzo ni dereva wa lori lililobeba vinywaji ambaye alitaka kulipita gari lililokuwa mbele yake na hivyo alianza kuyumba na kupoteza uelekeo, kisha kuligonga basi hilo.
Kipande amesema amesema baada ya ajali hiyo, alifanikiwa kutoka akiwa na majeraha na kukimbizwa hospitali ambako alipata huduma ya kwanza na baadaye kuingizwa kwenye chumba cha upasuaji kwa ajili ya kushonwa eneo la paji la uso ambalo alipasuka.
“Nilikuwa nakwenda Dar es Salaam kusalimia familia yangu, maana ni muda mrefu nilikuwa sijaenda kuwaona. Kikweli namshukuru Mungu kwa kutoka salama kwenye ajali hii, nilishuhudia wenzangu wakitoka wakiwa wamekufa,” amesema Kipande.
Ameongeza kuwa “Tayari familia yangu imeshapata taarifa hizi na nitakaporuhusiwa nitakwenda Dar es Salaam kuangalia hali ya afya yangu itakavyoendelea. Nimeumia sehemu za kichwa, hivyo nahitaji muda wa kupumzika ili afya yangu itengemae.”