WMA, TAKUKURU WATEKELEZA MAELEKEZO YA RAIS SAMIA

Mgeni Rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Kaspar Mmuya, akizungumza wakati akifungua semina kuhusu matumizi ya vipimo sahihi iliyoandaliwa na Wakala wa Vipimo (WMA), Mkoa wa Dodoma kwa watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Septemba 06, 2024 jijini Dodoma.

Na Veronica Simba, WMA Dodoma

Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma imetoa elimu ya vipimo kwa Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), hivyo kutimiza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayozitaka Mamlaka na Taasisi za Umma kupanga na kutekeleza kwa pamoja majukumu mbalimbali ya Serikali.

Akifungua Semina hiyo ya siku moja iliyofanyika jijini Dodoma, Septemba 6, 2024, Katibu Tawala wa Mkoa, Kaspar Mmuya amepongeza ushirikiano wa Taasisi hizo mbili unaolenga kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais na kuwahudumia wananchi ipasavyo.

“Nimefurahishwa na ushirikiano wa Taasisi hizi mbili wenye lengo la kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhusu dhana ya kufikiri kwa pamoja na kutenda kwa pamoja kama Serikali.”

Aidha, Katibu Tawala Mmuya amewataka washiriki kutumia semina hiyo kupambanua endapo kuna mapungufu yoyote katika Sheria ya Vipimo inayosimamiwa na WMA na kutafuta suluhisho la pamoja ili kuboresha utekelezaji wake.

Vilevile, amewataka WMA kuendelea kutoa elimu ya vipimo kwa wafanyabiashara na walaji ili pande zote mbili zipate kilicho stahiki. Pia, ameongeza kwamba katika utoaji elimu, wakulima waeleweshwe kuachana na utamaduni wa kutumia madalali bali wauze mazao yao katika maghala.

“Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo kwamba mazao yauzwe kwenye maghala na huko kwenye maghala kuwe na mizani ambazo zimekaguliwa na kuhakikiwa na Wakala wa Vipimo ili kumlinda mlaji na mfanyabiashara,” ameeleza Mmuya.

Mmuya ametoa wito kwa wafanyabiashara, walaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi na kuwakumbusha kwamba sheria ya vipimo imewapa WMA mamlaka ya kutoza faini kwa yeyote atakayekiuka mwongozo wa sheria hiyo.

Amewataka WMA na TAKUKURU kuwa mfano kwa sheria wanazozisimamia na kuchukuliana hatua baina yao endapo kutabainika ukiukwaji wa sheria.

“TAKUKURU, mtumishi yeyote wa WMA akitenda ndivyo sivyo kwa kujihusisha na rushwa basi achukuliwe hatua, vivyo hivyo kwa WMA, mkibaini mtumishi wa TAKUKURU anajihusisha na uvunjifu wa sheria ya vipimo katika shughuli zake kama mtanzania wa kawaida ikiwemo kilimo, biashara na nyinginezo, msisite kumchukulia hatua,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma, Karim Zuberi amesema lengo la kutoa semina hiyo kwa watumishi wa TAKUKURU ambao ni watumiaji wa vipimo, ni kuwapatia uelewa ili wajue haki zao wanaponunua bidhaa au kupata huduma mbalimbali.

“Kupitia semina hii watapata uelewa ni kwa namna gani kipimo kinatakiwa kuwa kabla, wakati na baada ya kununua bidhaa au kupata huduma,” amesema Zuberi.

Vilevile, amesema malengo mengine ni kutekeleza moja ya majukumu ya WMA ambalo ni utoaji elimu ya vipimo kwa jamii kupitia makundi mbalimbali kama wafanyabiashara, viongozi, wanasiasa, watumishi wa umma na mengineyo ambapo TAKUKURU ni kundi mojawapo.

Amesema, lengo jingine ni kupata maoni ya TAKUKURU kuhusu namna bora ya kutekeleza sheria ya vipimo endapo watabaini mapungufu wakati wa uwasilishwaji mada katika semina husika.

Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Victor Swela ameishukuru WMA kuona umuhimu wa kuandaa semina hiyo ili kuwajengea uelewa wa masuala ya kivipimo hivyo kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kiufanisi katika sekta hiyo.

“Tutashirikiana na wenzetu wa WMA kuwaelimisha wananchi na kusimamia kuhakikisha kila upande unazingatia matumizi ya vipimo sahihi kwa manufaa ya pande zote yaani wafanyabiashara na walaji.”

Mgeni Rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Kaspar Mmuya, akizungumza wakati akifungua semina kuhusu matumizi ya vipimo sahihi iliyoandaliwa na Wakala wa Vipimo (WMA), Mkoa wa Dodoma kwa watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Septemba 06, 2024 jijini Dodoma.

Meneja, Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma, Karim Zuberi akizungumza wakati wa semina kuhusu matumizi ya vipimo sahihi iliyoandaliwa WMA, kwa watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Septemba 06, 2024 jijini Dodoma.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma, Victor Swela akizungumza wakati wa semina kuhusu matumizi ya vipimo sahihi iliyoandaliwa na Wakala wa Vipimo (WMA), Mkoa wa Dodoma kwa watumishi wa TAKUKURU, Septemba 06, 2024 jijini Dodoma.

Sehemu ya watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa semina kuhusu matumizi ya vipimo sahihi iliyoandaliwa na Wakala wa Vipimo (WMA), Mkoa wa Dodoma kwa watumishi wa TAKUKURU, Septemba 06, 2024 jijini Dodoma.

Related Posts