BAADA ya kutumika zaidi ya miaka 10 mfululizo, beki wa zamani wa Simba na Yanga, Kelvin Yondani amesema amejipa likizo ya muda kujihusisha na masuala ya soka, ila hajaamua kustaafu kwa sasa, huku akikiri Ligi Kuu Bara kwa sasa imekuwa na ubora na ushindani mkubwa akiitaja Yanga na moto iliyonayo.
Beki huyo wa kimataifa wa Tanzania, msimu uliopita aliicheza Ligi Kuu Bara akiwa na Geita Gold iliyoshuka daraja hadi Ligi ya Championship, huku akimaliza mkataba na klabu hiyo, aliliambia Mwanaspoti kwa simu anasikilizia kwanza huku akipumzisha mwili na akili kwa muda kabla ya kurejea tena.
“Mpira ni burudani, lakini akili kubwa na nguvu zinatumika ili kuonyesha ubora, hivyo kutokana na kutumika kwa muda mrefu nakula pensheni kwanza, muda wa kucheza ukifika nitafanya hivyo,” alisema Yondani mwenye umri wa miaka 39 na kuongeza;
“Sijastaafu nimepumzika na nilikuwa na ofa nyingi kutoka timu zinazoshiriki Ligi Kuu na Championship lakini niliwaambia napumzika siwezi kuzitumikia timu zao. Bado nina nguvu na uwezo wa kucheza kwa muda zaidi kwa nafasi yangu ya beki ya kati.”
Akizungumzia ligi kwa jumla, Yondani alisema msimu ulioisha ulikuwa mzuri na wa ushindani bahati mbaya kwao walishindwa kuendana na kasi na kujikuta wakishusha timu.
“Msimu ulioisha nikiwa na Geita nilikutana na mikiki mikiki, kwani ulikuwa msimu bora na wa ushindani, bahati mbaya tulishindwa kuonyesha ubora na kujikuta tunaishusha timu, naamini mipango inayoendelea juu ya timu hiyo wanaweza kurudi msimu ujao,” alisema Yondani aliyewahi kukipuiga pia Polisi Tanzania na Taifa Stars.
Aliongeza ubora uliopo kwenye ligi hiyo, Yanga imeweza kuendana na kasi ikitwaa mataji mfululizo na kujenga kikosi imara na bora ambacho kinapambana kujiweka kwenye nafasi nzuri kimataifa.
“Yanga ya misimu mitatu iliyoisha na ikitwaa mataji yote, ni bora na inaimarika. Imejitosheleza kwenye ushindani wa ndani na sasa inapenya kimataifa, naiona mbali,” alisema Yondani aliyeanza kufahamika akiwa jijini Mwanza miaka ya mwanzoni mwa 2000 akiwa na Mwanza United kabla ya kusajiliwa na Simba mwaka 2006 aliyoichezea hadi 2012 na kuhamia Jangwani alikokaa hadi mwaka 2020 kabla ya kutua Polisi Tanzania 2021.